Germany: Jinsi ya kuilinda Mahakama ya Juu
6 Machi 2024Wanasheria na wanasiasa nchini Ujerumani wanaandaa mipango ili kuilinda mahakama ya juu ya nchi dhidi ya uwezekano wa kuhujumiwa, endapo serikali zinazopinga demokrasia zitaingia madarakani mnamo siku za usoni, baada ya kutukia utata katika nchi mbili ambazo pia ni wanachama wa Umoja wa Ulaya. nchi hizo ni Hungary na Poland.
Mafanikio ya chama cha mrengo mkali wa kulia, kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani, (AfD) kinachozingatiwa kuwa na pande zinazotishia katiba ya nchi, yamewatanabahisha watu nchini humo.
Soma pia:Ujerumani yakanusha kuitishwa kwa balozi wake Moscow
Chama hicho kwa sasa kinafikia asilimia 20, nchini kote, katika utafiti wa kura za maoni.
Baraza la shiriklisho ambalo ni tawi la bunge linalowakilisha majimbo yote 16 ya Ujerumani tayari limeshatayarisha mswada wa sheria wenye kurasa 14 kwa lengo la kuweka msingi wa sheria zitakazotumiwa na mahakama ya katiba, kuzizuia serikali zijazo kufanya mabadiliko ya katiba.
Katiba ya Ujerumani inasemaje?
Katiba ya Ujerumani ambayo ni sheria inajumuisha ibara tatu zinazoamua jinsi mahakimu 16 wa mahakama ya katiba wanavyoteuliwa. Kwa sasa nusu ya majaji hao wanateuliwa na bunge la Ujerumani na wengine wanateuliwa na baraza la shirikisho ambalo ni tawi lingine la bunge linalotokana na majimbo yote 16 ya Ujerumani.
Hata hivyo, kulingana na mswada wa sheria, yapo mapengo ya kutiliwa maanani katika katiba yanayotishia uhuru wa mahakama. Kwa mfano hakuna ulazima wa kupatikana thuluthi mbili ya kura ili kuwateua majaji wapya. Pia hakuna kikomo cha mihula na kwamba hakuna utaratibu wa kupiga marufuku majaji hao kuteuliwa tena.
Soma pia: Scholz aahidi uchunguzi wa haraka kuhusu udukuzi wa Urusi
Ndiyo kusema endapo serikali ya madikteta itaingia madarakani, mnamo siku za usoni itawezekana kwa madikteta hao kupunguza idadi ya kura zinazohitijika ili kuweza kuwateua mahakimu wanaoegemea upande wa serikali.
Mswada wa sheria wa baraza la shirikisho la Ujerumani unalenga shabaha ya kuondoa uwezekano wa wabunge wachache au thuluthi moja ya wabunge kuweza kupinga uteuzi wa majaji na hivyo kuivunja nguvu kabisa mahakama ya juu ya nchi.
Sheria za kuteua majaji wapya
Mgogoro uliosababishwa na mageuzi ya mahakama nchini Poland hivi karibuni, umewapa nguvu wanasheria wengi nchini Ujerumani ya kutafuta njia za kuilinda mahakama ya katiba ambayo ni mahakama ya juu kabisa hapa nchini.
Mgogoro huo wa nchini Poland uliochochea maandamano makubwa, ulianza mnamo mwaka 2015 baada ya chama tawala cha nchi hiyo, cha "sheria na haki”, (PiS) kilipolaumiwa kwa kujaza mahakimu wao. Kutokana na kuwa na wabunge wengi, chama hicho kiliweza kubadilisha sheria ili kuwateua majaji wapya.
Soma pia: Jeshi la Ujerumani kwenda bahari ya Shamu
Hata hivyo baadhi ya wataalamu wa masuala ya sheria wanatoa angalizo juu ya mswada wa sheria wenye lengo la kuilinda mahakama ya katiba nchini Ujerumani. Mtafiti mwandamizi kwenye chuo kikuu cha Kiel, Stefan Martini amesema, mageuzi ni jambo zuri lakini inapasa kuzingatia misingi ya sheria.
Mtaalamu huyo amesema kuzifanya sheria ziwe ngumu kubadilishwa sio suluhisho kwa sababu ikiwa serikali ya mrengo mkali inaondoka madarakani na ya kidemokrasia inaingia, serikali hiyo pia itahitaji kuwa na wabunge wengi ili kuweza kubadilisha sera.