Ujerumani yakanusha kuitishwa kwa balozi wake Moscow
4 Machi 2024Kwenye mahojiano na shirika la habari la Ujerumani, DPA, Alexander Graf Lambsdorff, balozi wa Ujerumani huko Moscow amesema alikuwa na mazungumzo kuhusu maswala ya nchi hizi mbili katika wizara ya mambo ya nje ya Urusi. Alikanusha madai ya kwamba aliitishwa ili kujieleza na kusema kulikuwa na mwaliko wa kujadili masuala mbalimbali baina ya Ujerumani na Urusi. Lakini balozi huyo hakutoa maoni yoyote kuhusu maudhui maalum ya mazungumzo hayo ya leo.
Miadi ya muda mrefu ?
Christian Wagner, msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani pia aliweka wazi kuwa balozi huyo alikuwa wizarani kwa miadi iliyopangwa muda mrefu uliopita.
"Kwa kweli, balozi wetu alikuwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi asubuhi ya leo kwa miadi ambayo tayari ilikuwa imepangwa kwa muda. Katika suala hili, nitasema kwamba hakuiitishwa ili kujieleza. Siwezi kuzungumzia kwa undani juu ya yaliyojadiliwa hapo.", alisema Wagner.
Kauli hiyo ni kinyume na taarifa ya vyombo vya habari vya Urusi. Shirika la habari la serikali ya Urusi TASS liliripoti asubuhi ya leo kuwa balozi wa Ujerumani aliitwa na wizara ya mambo ya nje ya Urusi kufuatia kuvujishwa kwa nyaraka za siri za maafisa wa jeshi la Ujerumani kuhusu vita nchini Ukraine na uwezekano wa Ujerumani kupeleka makombora ya masafa marefu ya Taurus nchini humo.
Urusi haishangazwi na maudhui ya nyaraka za siri za Ujerumani
Serikali ya Urusi imesema leo Jumatatu kwamba nyaraka hizo za siri zilizovujishwa zinaonyesha ushiriki wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi katika mzozo wa Ukraine. Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema maudhui ya nyaraka hizo za siri haishangazi mtu yeyote.
''Inawezekanaje kwamba mtandao wa mawasiliano salama haukuwa wa kutegemewa sana? Na hiyo inamaanisha mengi. Majenerali hao, labda, pia walipata aina fulani ya neno sahihi ili kuhalalisha katika nyanja ya umma wazo la kutuma vikosi vya ardhini vya nchi binafsi wanachama wa NATO, wamekuwa wakizungumzia uwezekano wa kutuma nchi za NATO kwa sasa.'', alithibitisha Lavrov.
Akiwa ziarani huko Montenegro, leo Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema nchi yake inapaswa kutathmini uwezekano wowote linapokuja suala la kuisaidia Ukraine lakini msimamo wa Ujerumani ni wazi kuhusu kupeleka makombora ya Taurus nchini Ukraine. Akiimanisha kwamba nchi yake haitofanya hivyo.
Vyanzo: DPA, AFP