1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yawapokea wahamiaji

12 Juni 2018

Shirika moja la misaada limesema hii leo kwamba mamia ya wahamiaji waliokwama kwenye meli ya uokozi katika bahari ya Mediterania watapelekwa nchini Uhispania, kwa msaada wa meli mbili za Italia.

https://p.dw.com/p/2zLcd
Spanien Ankunft gerettete Flüchtlinge in Malaga
Picha: Reuters/J. Nazca

Shirika moja la misaada limesema hii leo kwamba mamia ya wahamiaji waliokwama kwenye meli ya uokozi katika bahari ya Mediterania watapelekwa nchini Uhispania, kwa msaada wa meli mbili za Italia, kufuatia hali mbaya ya hewa iliyosababisha hofu ya usalama wa wahamiaji hao. Hatua hiyo inafuatia mvutano uliozuka kati ya Malta na Italia ambazo zilikataa meli hiyo kutia nganga katika bandari zao.

Wahamiaji 629, ambao ni pamoja na wanawake wajawazito na watoto wengi wamejikuta katikati ya mvutano mkali kati ya Malta na Italia, tangu baada ya kuokolewa na meli ya uokozi ya Ufaransa ya SOS Mediteranee mnamo siku ya Jumamosi. Malta na Italia walikataa kuiruhusu meli hiyo kutia nanga.

Serikali mpya ya Uhispania chini ya waziri mkuu Pedro Sanchez, hatimaye iliruhusu meli hiyo kutia nanga katika bandari yake ya mashariki ya Valencia, na kusisitiza kwamba ilikuwa ni wajibu wa kiutu kufanya hivyo.

Mashirika ya kutoa huduma za misaada wameelezea wasiwasi wao kwamba meli hiyo huenda isingweza kufika salama Uhispania kutokana na kuvurugika kwa hali ya hewa. Lakini pia walionyesha wasiwasi wao kuhusu uwezo wa meli hiyo iliyokuwa na uwezo wa kusafirisha takriban abiria 500, ambayo isingeweza kubeba abiria 629 waliookolewa na kufika salama bandarini.

Miongoni mwa wahamiaji waliokuwa kwenye meli hiyo, 7 walikuwa ni wanawake wajawazito, watoto 11 na watoto wengine 123 ambao hawakuwa na watu waliowasindikiza.

Italien Flüchtlinge in Augusta
Meli ya uokozi ya Ufaransa iliyowaokoa wahamiaji hao kwenye bahari ya MediteraniaPicha: Reuters/A. Parrinello

Mapema hii leo, waokozi kutoka Italia walijitolea kusaidia kuwahamisha wahamiaji hao na kuwapeleka Uhispania, huku meli moja ya Italia ikiwasilisha misaada mbalimbali kwenye meli hiyo inayosubiri kuondoka kutoka kwenye eneo la bahari la Malta.

Malta na Italia kwa pamoja zimeishukuru Uhispania kwa kufikia hatua hiyo, laki wakiendeleza mzozo wao juu ya nani aliyekuwa na jukumu la kuwapokea. Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini aliandika "ushindi" kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte alisema nchi yake iliomba kile alichosema ishara ya mshikamano kutoka Umoja wa Ulaya na ishara hiyo ilionyeshwa. Conte anatarajiwa kuelekea Paris kwa mazungumzo na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron mnamo siku ya Ijumaa, kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya Juni 28-29, utakaozungumzia masuala ya uhamiaji, ofisi ya Macron imesema jana Jumatatu.

Waziri mkuu wa Malta Joseph Muscat nae aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter akielekeza shukrani zake kwa Sanchez kwa kukubali kuiruhusu meli hiyo baada ya Italia kukiuka sheria za kimataifa na kusababisha hamaki kubwa. Aliongeza kuwa itakuwa ni muhimu kukaa pamoja na kujadiliana, ili kuepusha suala kama hili kutokea tena huko mbeleni.

Waziri mkuu huyo wa Uhispania amesema, kufuatia hatua hiyo ya kukubali kuwapokea wahamiaji, nchi yake inatarajia kuwashinikiza viongozi wa Umoja wa Ulaya kujadili kwa kina sera za umoja huo zinazohusu uhamiaji baadae mwezi huu. 

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman