Uamuzi wa Italia unaweza kuathiri sheria za uhamiaji Ulaya?
15 Juni 2018Serikali mpya ya siasa kali za mrengo wa kulia inayopinga uhamiaji ya Italia imechukua hatua isiyo ya kawaida ya kuzuia boti iliyowabeba wahamiaji kutia nanga katika bandari zake, jambo ambalo limepongezwa na viongozi wenye misimamo mikali kuhusu uhamiaji nchini Austria.
Matteo Salvini, naibu waziri mkuu mpya wa Italia na waziri wa mambo ya ndani, anayeongoza chama kinachopinga uhamiaji Jumapili iliyopita aliizuia meli ya msaada ya Aquarius, iliyokuwa imebeba wahamiaji 629 kutia nanga kwenye bandari za Italia.
Salvini alisisitiza kwamba kuizuia meli hiyo kulikuwa kwa makusudi na kulilenga kukumbushia mshikamano thabiti miongoni mwa washirika wa Umoja wa Ulaya katika kukubali mgawanyo sawa wa wahamiaji wanaoingia kupitia njia ya baharini.
Salvini alisema kwenye mahojiano na shirika la utangazaji la La7 Jumanne iliyopita lisema, siyo sera mbaya, ni kutumia akili tu. Alisema na hapa namnukuu, "tunataka kuokoa maisha ya watu, lakini pia kushirikiana kuubeba mzigo wa wahamiaji katika kiwango cha Umoja wa Ulaya, na si kwa Italia peke yake.
Hadi ilipofika siku ya Ijumaa, ikiwa ni takriban wiki moja baada ya kuokolewa, meli hiyo ya Aquarius iliyokuwa na wahamiaji ilikuwa bado ikielea baharini, ikiwa na mamia ya wahamiaji, ambao miongoni mwao waliugua hasa hali ya hewa inapoharibika, wakiwa safarini kuelekea Uhispania, ambako serikali yake ilikubali meli hiyo kutia nanga kwenye bandari yake ya Valencia.
Pwani za Italia, hapo awali zilifungua milango yake kwa wahamiaji waliookolewa kutoka bahari ya Mediterania: tangu mwaka 2014, taifa hilo limeshuhudia zaidi ya wahamiaji 640,000 wakiingia kwenye pwani zake. Idadi hiyo inalinganishwa na wahamiaji takriban milioni 1.1 walioingia Ugiriki na zaidi ya 50,000 nchini Uhispania, hii ikiwa ni kulingana na taarifa zilizotolewa na Umoja wa Mataifa.
Salvini alishinda idadi kubwa ya kura kwenye uchaguzi wa Italia mwaka huu bada ya kuahidi kulinda mipaka yake na kuwaondosha karibu wahamiaji haramu 500,000. Huku akikabiliwa na shinikizo la kutekeleza ahadi hiyo, ametolea mfano wa meli hiyo ya Aquarius na tangu hapo amepata sifa kubwa, lakini akilaumiwa vikali na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Hungary na Slovakia mataifa mawili ambayo yaligoma kutekeleza sera ya Umoja wa Ulaya ya kushirikiana kubeba mzigo wa wahamiaji, walisifu hatua hiyo ya Italia. Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban alisema Jumanne iliyopita kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba "Ni hatua kubwa, ninawatakia mafanikio mema Italia na tuko nyuma yao.”
Kulingana na mchambuzi katika Umoja wa Ulaya Stefano Torelli, uamuzi huo wa Italia unaweza kuua matarajio ya kuimarisha mshikamano wa Umoja wa Ulaya kwenye masuala yahusuyo uhamiaji na makaazi. Amesema itazamisha kabisa majaribio ya kufufua upya mipango ya kuwahamisha wahamiaji, mpango ambao ni wa karibuni zaidi unaolenga kupunguza mzigo wa wakimbizi nchini Italia.
Mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR Filippo Grandi, yeye amesema ameona hatari ya muda mrefu juu ya maamuzi hayo dhidi ya Aquarius, na kuonya kwamba kuizuia meli kutia nanga huenda pia ukazifanya meli za uokozi kuacha kuwaokoa wahamiaji wanaokwamba baharini huko mbeleni.
Kilio cha wahamiaji kimeibua maswali mengi kuhusu uzalendo na wajibu wa kiutu. Je hatua hiyo ya kikatili ya Italia iliyopingwa na Ufaransa na kutajwa kuwa ni ya kukwepa majukumu, lakini pia hatua ya Uhispania, kwa namna yoyote zinaweza kuyabadilisha mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya na namna wanavyowahudumia watu wanaoomba makazi?
Huenda pasiwe na uwezekano huo, amesema Zsolt Darvas, mjumbe mwandamizi kwenye jopo la wataalamu washauri wa kiuchumi lililopo mjini Brussels. Amesema maamuzi kuhusu watu wanaoomba makazi yanatofautiana sana miongoni mwa mataifa wanachama. Kwa miaka mitatu iliyopita, Hungary na Poland kwa wastani walikubali takriban asilimia 10 hadi 20 ya waomba makazi. Mataifa mengine yalikuabli hadi asilimia 80. Baadhi ya mataifa yako wazi, lakini mengine hupendelea zaidi kukataa maombi hayo, alisema Zarvas.
Wakati hayo yakiendelea, viongozi wa Umoja wa Ulaya watakutana mjini Brussels ifikapo Juni 28 hadi 29, na ajenda kuu itakayojadiliwa ni mipango ya muda mrefu iliyosimama ya kutengeneza upya kanuni ya Umoja wa Ulaya kuhusu maombi ya ukaazi na uhamiaji, lakini kukiwa na matarajio finyu kuhusu kufikiwa kwa suluhu.
Mwandishi: Lilian Mtono, dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman