UAE: Watatu wafa katika mlipuko
17 Januari 2022Watu watatu wamekufa na wengine wamejeruhiwa kwenye shambulizi la ndege zisizokuwa na rubani katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Shambulizi hilo lililohisiwa kulenga visima muhimu vya mafuta katika mji mkuu Abi Dhabi lilisababisha pia moto katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abu Dhabi mapema hii leo.
Waasi wa Kihouthi wa nchini Yemen wamekiri kufanya shambulizi hilo mara baada ya mamlaka za Abu Dhabi kuripoti matukio mawili ya moto katika mji huo mkuu. Polisi mjini Abu Dhabi imesema malori matatu ya mafuta yalishika moto katika eneo la viwanda la Musaffah, karibu na ghala la shirika la mafuta la ADNOC. Aidha kituo cha ujenzi kilichopo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abu Dhabi pia kilishika moto
Shirika la habari la serikali limeripoti kuwa watu watatu ambao ni raia wawili wa India na mmoja wa Pakistan wamekufa na sita wamejeruhiwa katika shambulio hilo.
Jeshi la polisi limesema wakati uchunguzi ukiendelea, tathmini ya awali inaonyesha kulikuwepo na vifaa vidogo vilivyokuwa vikipaa angani, na huenda vikawa ni vya ndege hizo zisizotumia rubani, ambavyo viliangika katika maeneo mawili na huenda ndivyo vilivyosababisha mlipuko na moto. Imesema, hakukua na uharibifu mkubwa uliosababishwa na tukio hilo, ingawa hawakueleza zaidi.
Wanamgambo hao wa Houthi hata hivyo hawakueleza kwa kina kuhusiana na uhusika wao kwenye shambulizi hilo. Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran huko nyuma liliwahi kudai kufanya mashambulizi kadhaa, ingawa maafisa wa Emirati walikana kwamba yaliwahi kutokea.
Wachambuzi waonya kupatikana suluhu ya kikanda kuepusha mashambulizi kama hayo.
Mchambuzi kiongozi katika kampuni ya kiintelijensia ya Verisk Mapleroft Tobjorn Soltvedt amezungumzia shambulizi hili, huku akionya mataifa ya eneo hilo kusaka suluhu ya haraka ya kumaliza mivutano, ili kuzuia kitisho kinachoendelea baina yao.
Amesema "Shambulizi hili linatukumbusha kitisho cha mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani nchini UAE na eneo zima ambako tumeona mifano kadhaa ya mashambulizi kama hayo, kama Saudi Arabia. Na kwa kweli changamoto kwa UAE na kwa Saudi Arabia na wengine katika ukanda huo ni kwamba kama ahawataweza kupata njia ya kusuluhisha mivutano ya kikanda na kuzuia uhasama baina ya serikali za kikanda na wahusika wengine, ni wazi kitisho hiki kitaendelea".
Soma Zaidi: Wahouthi washambulia viwanja vya ndege vya Saudi Arabia
Shambulizi hilo linafanyika wakati vita vya muda mrefu vikiendelea kuitafuna Yemen pamoja na hatua ya wanamgambo wa Houthi hivi karibuni kuikamata meli iliyokuwa na bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Ingawa Abu Dhabi kuwa tayari imeyaondoa majeshi yake kwa kiasi kikubwa kwenye vita hivyo vilivyoliharibu vibaya Yemen, taifa masikini kabisa kwenye ulimwengu wa Kiarabu, lakini bado inajihusisha kwa kuwasaidia wanamgambo wa Yemen wanaopambana na Houthi.
Soma Zaidi: Marekani yalaani shambulio la kundi la waasi wa Houthi dhidi ya Saudi Arabia
Hata hivyo tukio la uwanja wa ndege kulingana na polisi lilikuwa ni dogo tu na lilitokea kwenye eneo ambako ujenzi ulikuwa ukiendelea. Shirika na ndege la Etihad, ambalo Abu Dhabi ndio uwanja wa nyumbani limesema lilichukua hatua za tahadhari kutokana na athari ndogo zilizosababishwa mvurugiko wa safari chache, lakini baadae safari zilirejea kama kawaida.
Mashirika: APE/AFPE