1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi wadai kuteka maelfu ya wanajeshi wa Saudi Arabia

Daniel Gakuba
29 Septemba 2019

Waasi wa Kihouthi nchini Yemen wamedai wamefanya shambulizi kubwa karibu na mpaka wa nchi hiyo na Saudi Arabia, na kuchapisha picha za magari yanayowaka moto, na wanajeshi wengi wanaojisalimisha katika eneo la milima.

https://p.dw.com/p/3QRyQ
Jemen Kämpfer der Houthi-Rebellen
Wapiganaji wa Kihouthi kwenye uwanja wa vitaPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Hayo yanafuatia tangazo la hapo jana la kuwachukua mateka maelfu ya wanajeshi wa Saudia Arabia, madai ambayo hayajathibitishwa wala kukanushwa na Saudi Arabia.

Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi Yahia Sarie alisema katika tangazo lilirushwa na kituo cha televisheni cha waasi hao cha Al-Masirah, kwamba ''brigedi tatu za maadui'' zimeangushwa katika shambulizi lililofanyika saa 72 kabla ya tangazo hilo kutolewa. Aidha, msemaji huyo aliongeza kuwa mashambulizi yao yalisaidiwa na ndege zisizo na rubani pamoja na mfumo wao wa ulinzi wa anga.

Wahouthi wadai kuwauwa Wasaudia 500

Kulingana na tangazo hilo, ''maelfu'' ya wanajeshi wa adui zao walichukuliwa mateka, miongoni mwao wakiwemo maafisa wa jeshi la Saudi Arabia, na mamia ya magari ya kivita. Vile vile limedai kuwa wanajeshi 500 wa Saudi Arabia wameuawa katika operesheni hizo.

Jemen Yahya Sarea in Sanaa
Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi Yahia SariePicha: Reuters

Msemaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Wahouthi hakujibu mara moja, alipoulizwa na shirika la habari la Reuters, kauli yake kuhusiana na madai ya waasi hao. Shirika hilo halikuweza kuthibitisha uhalisia wa taarifa za Wahouthi za kuwakamata maelfu ya wanajeshi wa Saudi Arabia.

Mnamo miezi ya hivi karibuni, vikosi vya Yemen vinavyoungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia vimekuwa vikiwashambulia Wahouthi katika eneo la Kafar kwenye mkoa wa Kaskazini wa Saada karibu na mpaka wa Saudi Arabia. Wenyeji wa eneo hilo wamearifu kuwa Wahouthi wamewakamata wanajeshi wengi wa serikali katika mapigano hayo.

Majibu kwa hujuma za anga na nchi kavu

Taarifa ya Wahouthi kupitia televisheni yao imesema mashambulizi ya hivi karibuni ni jibu kwa hujuma ambazo wamekuwa wakifanyiwa na Saudi Arabia na washirika wake kwa kipindi cha miaka minne sasa.

Ushirika huo wa nchi za Waislamu wa madhehebu ya Sunni ambao unasaidiwa na nchi za magharibi kwa silaha na taarifa za kijasusi uliingilia kati nchini Yemen mwaka 2015, baada ya Wahouthi kuukamata mji mkuu wa Yemen, Sanaa, na kuisambaratisha serikali ya nchi hiyo inayotambuliwa na Jumuiya ya kimataifa mwaka 2014.

Kukithiri kwa uhasama wa hivi karibuni ni pigo kubwa kwa juhudi za Umoja wa Mataifa kumaliza mivutano katika taifa hilo la Kiarabu, na kuanzisha mazungumzo ya amani kwa lengo la kuumaliza mzozo huo wa kivita ambao umesababisha vifo vya maelfu na kuwafanya mamilioni kuyakimbia makaazi yao.

dpae, rtre