1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi wadai kuhusika na mashambulio ya Buqyaq

Oumilkheir Hamidou
14 Septemba 2019

Hujuma za ndege zinazoruka bila ya rubani zimesababisha moto katika vituo viwili vya kampuni la mafuta la Saudi Arabia-Aramco, mashariki mwa nchi hiyo. Waasi wa Houthi wamedai kuhusika na hujuma hizo.

https://p.dw.com/p/3PbdV
Saudi-Arabien Feuer in der Aramco-Ölaufbereitungsanlage in Abkaik
Picha: Reuters

Waasi wa Houthi wenye mafungamano na Iran wanasema wamerusha ndege 10 zisizokuwa na rubani kufanya mashambulio dhidi ya vituo muhimu vya mafuta nchini Saudi Arabia.  Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani  ya Saudi Arabia, hujuma hizo zimesababisha moto katika vituo viwili vinavyosimamiwa na kampuni la mafuta la nchi hiyo, Aremco, katika mkoa wa mashariki wa Buqyaq. Kwa mujibu wa afisa huyo wa serikali, moto huo ulidhibitiwa baadae.

Msemaji wa wanamgambo wa Yemen amesema shambulio hilo "ni jibu" kwa opereshini za kijeshi zinazoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Houthi nchini Yemen.

Kituo cha kusafisjhia mafuta cha Abqaiq nchini Saudi Arabia
Kituo cha kusafisjhia mafuta cha Abqaiq nchini Saudi ArabiaPicha: AFP/STRINGER

Wanamgambo wa Houthi watishia kuzidisha makali ya mashambulio yao

"Tunaiahidi serikali ya Saudi Arabia opereshini itakaofuata itakwenda mbali zaidi  na itasababisha madhara makubwa zaidi" amesema msemaji huyo wa kijeshi wa wanamgambo wa Houthi aliyenukuliwa na kituo cha televisheni cha al Masirah kinachoelemea zaidi upande wa wa Houthi.

Buqyaq, mji ulioko umbali wa kilomita 330 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Saudi Arabia, Ryadh ni kitovu cha mtambo mkubwa zaidi wa kusafishia mafuta ulimwenguni-hayo lakini ni kwa mujibu wa kampuni ya Aramco.

Hadi wakati huu haijulikani bado kama hujuma hizo zimeathiri shughuli za kuchimba mafuta. Mnamo miezi ya hivi karibuni, wanamgambo wa Houthi wamekuwa wakizidisha hujuma za makombora na ndege zisizokuwa na rubani katika nchi jirani ya Saudi Arabia.

Yemen, mojawapo ya nchi masikini zaidi ya ulimwengu wa kiarabu inakabwa tangu mwaka 2014 na mapambano kati ya wahouthi na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia. Saudi Arabia inahofia wahouthi wasije wakawapatia mahasimu wao wakubwa katika eneo hilo, Iran, upenu wa kuimarisha ushawishi wake katika ulimwengu wa kiarabu.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri:Amina Mjahid