Tunisia: Wahamiaji walitumiwa dola bilioni 1 mwaka huu
15 Julai 2023Miamala hiyo imetajwa kuwa ilifanywa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023 pekee. Rais Kaes Saied aliyekuwa mwenyekiti katika kikao hicho alionesha kushtushwa na kiwango hicho na amesema kuwa hilo linaonesha kwamba Tunisia inatumiwa kimalengo, na kwamba suala hilo linadhamiria kubadilisha muundo wa idadi na asili ya watu wa nchi hiyo, maoni ambayo yalikosolewa vikali na makundi ya haki za binadamu.
Soma zaidi:Tunisia yawalazimisha mamia ya wahamiaji kuondoka
Kiasi hicho cha fedha walichotumiwa wahamiaji wasio na vibali ni kikubwa kuliko mapato ya sekta ya utalii ya taifa hilo katika nusu ya kwanza ya mwaka ambayo yalikuwa ni dinari bilioni 2.2
Katika miezi ya hivi karibuni, maelfu ya wahamiaji kinyume cha sheria wamekuwa wakifurika katika mji ulio Pwani wa Sfax kwa madhumuni ya kusafiri kwa boti kuelekea Ulaya. Boti hizo ni zile zinazomilikiwa na walanguzi wa binadamu hatua ambayo imesababisha kutokea mwa mgogoro wahamiaji Tunisia.
Nchi hiyo, iliwaondoa kwa nguvu mamia ya wahamiaji mwezi huu na kuwapeleka katika eneo lililojitenga linalopakana na Libya na Algeria baada ya vurugu zilizotokea kati ya wakaazi na wahamiaji kwenye mji huo wa Sfax.
Kutokana na shinikizo la makundi ya ndani na ya kimataifa ya haki za binadamu yaliyozituhumu mamlaka nchini humo kwa kuweka maisha ya wahamiaji hatarini, serikali iliwahamishia katika makazi maalumu katika miji wiki hii.
Wahamiaji wengine bado wamekwama mipakani.
Jana Ijumaa, msemaji wa Jukwaa la haki za uchumi na jamii wa Tunisia Romdane Ben Amor aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kati ya wahamiaji 100 na 150 wakiwemo wanawake na watoto bado wamekwama kwenye mpaka wa nchi hiyo na Libya.
Aliongeza kuwa, karibu wahamiaji 165 walikuwa wametelekezwa karibu na mpaka wa Tunisia na Algeria bila ya kuweka wazi ni nani aliyewachukua na ni wapi walikopelekwa. Ben Amor amesema licha ya wahamiaji kuhamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine, makundi mengine hujificha mwituni kwenye mazingira magumu kwa kuhofia kuonekana na kuishia waliko wenzao waliokwama mipakani.
Ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Ulaya unatazamiwa kuwasili Tunisia Jumapili, ili kusaini mkataba unaoainisha msaada wa kifedha kwa ajili ya nchi hiyo ili kukabiliana na uhamiaji kinyume cha sheria.