Tume ya uchaguzi Kongo yafuta matokeo ya wagombea ubunge
6 Januari 2024Tume ya uchaguzi nchini Kongo imefuta kura zilizopigwa kwa wagombea 82 kati ya zaidi ya laki moja walioshiriki kwenye uchaguzi mkuu wa Desemba 20 kwa kuhusika kwao katika madai ya udanganyifu na masuala mengine ambayo yalivuruga uchaguzi.
Matokeo yaliyofutwa ni pamoja na ya wagombea wa ubunge, udiwani na uongozi wa manispaa ambayo matokeo rasmi bado hayajatolewa, hali ambayo inatishia kuiyumbisha zaidi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mzalishaji mkuu wa madini ya Kinywe (Kobalti) na nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika.
Taarifa ya Tume ya uchaguzi CENI ya mnamo Ijumaa jioni haikuzungumzia matokeo ya uchaguzi wa rais uliyofanyika wakati mmoja na chaguzi za bunge na madiwani. Matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa wiki iliyopita yalimpa Rais Felix Tshisekedi ushindi mkubwa, lakini upinzani umepinga matokeo hayo kwa madai ya kuwepo kasoro nyingi za uchaguzi zilizoripotiwa na wao wenyewe na wachunguzi wa kujitegemea.
Wagombea 82 waondolewa kwenye orodha ya wagombea
Tume ya CENI ilisema imeanzisha uchunguzi baada ya kuripotiwa na ''visa vya vurugu, uharibifu na hujuma uliofanywa na baadhi ya wagombea wenye nia mbaya dhidi yake, wapiga kura, wafanyakazi wao, mali zao na nyenzo za uchaguzi."
Uchunguzi huo umesababisha kufutwa kwa matokeo ya wagombea ubunge 82 pamoja na kubatilishwa kikamilifu kwa uchaguzi katika ngazi zote katika majimbo mawili ya uchaguzi kati ya 176. Majimbo hayo ni Masimanimba na Yakoma , magharibi na kaskazini magharibi mwa Kongo. Majimbo mengine 16 yalikuwa tayari yameondolewa kwenye uchaguzi kutokana na masuala ya usalama wa ndani huko Kivu ya Kaskazini na MaiNdombe.
Wakuu wa mikoa wanne, maseneta kumi na mawaziri watatu wa serikali walikuwa miongoni mwa wagombea 82 waliofutiwa matokeo na tume ya uchaguzi.
Hatua hiyo ya CENI haiwezi kuwaridhisha wapinzani wengi ambao wanaishutumu tume hiyo kwa kusaidia kurahisisha kuchaguliwa tena kwa Tshisekedi na kukataa madai yao kwamba matokeo ya uchaguzi yalivurugwa.
Wapinzani wakuu wa urais walitoa wito kwa wafuasi wao kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi. Mizozo ya uchaguzi mara nyingi huchochea machafuko nchini Kongo, ambayo maendeleo yake yametatizwa na miongo kadhaa ya utawala wa kimabavu, ufisadi, na mzozo wa usalama wa muda mrefu katika mikoa ya mashariki.
Je, kasoro ziliathiri pia matokeo ya uchaguzi wa rais ?
Tume ya uchaguzi CENI na serikali wamesema uchaguzi wa Desemba zaidi ulikuwa huru na haki licha ya kasoro hizo. Kasoro hizo ni pamoja na vituo vya kupigia kura kushindwa kufunguliwa siku ya uchaguzi, visa vya vurugu, ubovu wa mashine za kupiga kura na changamoto zingine zilisababisha kuongezwa kwa muda usioratibiwa wa upigaji kura ambao msingi wake wa kisheria umehojiwa na ujumbe mkuu wa waangalizi wa uchaguzi kutoka kanisa katoliki.
Tresor Kibangula, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kwenye taasisi ya utafiti kuhusu Kongo ya Ebuteli, amesema ilikuwa vigumu kuthibitisha ikiwa kasoro zilizotajwa na CENI hazikuathiri uchaguzi wa rais, "hasa ikizingatiwa kuwa kura hizi zote ziliendeshwa kwa njia moja siku na kifaa aina moja cha kielektroniki cha kupiga kura."
Kibangula lisema "swali kuu ni ... ikiwa kiwango cha ushindi wa Tshisekedi uliotangazwa kilipotoshwa na haya makosa ambayo yalionekana kuenea kote nchini
nchi.''