Rais Tshisekedi ashinda kura za awali za jiji la Kinshasa
28 Desemba 2023Hadi usiku wa kuamkia leo Tume ya Uchaguzi CENI, ilitangaza matokeo ya kura zaidi ya milioni 9 ambazo tayari zimehisabiwa. Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili ameonekana kupata kura zaidi ya milioni saba ambazo ni sawa na asilimia 77. Mpinzani wake wa karibu Moise Katumbi akiwa na asilimia 15 na Martin Fayulu akishika nafasi ya tatu na silimia 4 pekee.
Tshisekedi anaongoza kwa wingi wa kura katika majimbo 21 kati ya 26 ya Kongo pamoja na jiji kuu la Kinshasa. Huku Katumbi akiongoza katika majimbo manne ya kusini mashariki yakiwemo Haut-Katanga, Tanganyika, Lualaba na Haut-Lomami. Matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Rais yanatarajiwa kutangazwa jumapili ya Desemba 31.
''Kadima aliandaa machafuko ambayo hayawezi kufutwa na Mahakama ya Katiba''
Upinzani umeyapinga matokeo hayo ya awali na kusema yalipangwa na Tume ya uchaguzi ilikumpa ushindi Rais Tshisekedi. Olivier Kamitatu msemaji wa Moise Katumbi amesema uchaguzi lazima urudiwe na hawana dakika hata moja ya kuwasilisha malalamiko yao kwenye Korti ya Katiba.
''Vyombo vyote vinavyosimamia mchakato wa uchaguzi vinaongozwa na wanachama wanaohusishwa na kabila la Félix Tshisekedi. Kwa hivyo, Mahakama ya Kikatiba inaendeleza tu udanganyifu ambao tayari umepangwa.'', alisema Kamitatu.
Kabla ya kuendelea kusema : ''Kuwasilisha malamiko yetu kwenye mahakama hiyo ni kuhalalisha tu ulaghai wa mwenye kiti wa tume ya uchaguzi Denis Kadima. Bwana Kadima aliandaa machafuko ambayo hayawezi kufutwa na Mahakama ya Katiba, ambayo tayari yamekosolewa vikali kwa utendajikazi wake na hasa jaji mkuu wake.''
Patrick Muyaya, msemaji wa serikali alikosoa vikali kauli hiyo ya msemaji wa Katumbi na kusema upinzani unapanga kuandaa vurugu. Muyaya ameiambia DW kwamba machafuko hayata tokea na kuutaka upinzani kusubiri hadi matokeo kamili ya uchaguzi yatakapotolewa.
Polisi wafyatua gesi ya machozi kuwatawanya waandamanaji
Jana polisi mjini Kinshasa walitumia nguvu na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wachache katika wilaya ya Kasavubu. Mgombea wa urais Martin Fayulu, kiongozi aliyehamasisha maandamano hayo, ameilaumu polisi akidai wametumia risasi za moto na kwamba watu 11 wamejeruhiwa vibaya.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka kanisa katoliki na kanisa la kiprotestanti nchini wanatarajiwa kutoa baadae leo ripoti yao ya pamoja kuhusu uchaguzi huo. Zaidi ya waangalizi 36.000 kutoka makanisa hayo mawili walichunguza mchakato wa uchaguzi huo kote nchini Kongo.