1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kongo yapinga maandamano ya upinzani Kinshasa

27 Desemba 2023

Waziri wa Mambo ya ndani wa Kongo, Peter Kazadi amesema maandamano yaliyopangwa na wapinzani hii leo hayana msingi wa kisheria na yanalenga kuvuruga kazi ya tume ya uchaguzi CENI.

https://p.dw.com/p/4acGn
Kinshasa, Kongo | Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mgombea wa Urais Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mgombea wa Urais Felix Tshisekedi Picha: Pool Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance

Kazadi amesema serikali haitokubali maandamano kufanyika na upinzaniunapaswa kusubiri hadi matokeo kamili yatakapotolewa kuliko kuamua kuandamana. 

Hapo jana wagombea wa upinzani walisema wataendelea na mipango yao ya kufanya maandamano hii leo licha ya katazo hilo la serikali. 

Mmoja ya wagombea hao Martin Fayulu amesema yeye na wenzake wote walioitisha kwa pamoja maandamanao makubwa kulalamikia dosari za uchaguzi huo mkuu wataendelea na mipango hiyo kwa kuwa wanaamini uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu. 

Soma pia:Upinzani kuandamana Kongo licha ya marufuku ya serikali

Wameikosoa hatua ya CENI kurefusha zoezi la uchaguzi katika vituo vya kupigia kura ambavyo havikufunguliwa siku ya uchaguzi wakisema hatua hiyo ni kinyume cha katiba na kutaka uchaguzi urudiwe upya. 

Hadi sasa matokeo ya awali yaliotolewa na CENI baada ya zoezi la kura kufanyika Desema 20, yanamuonesha Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili anaongoza kwa idadi kubwa ya kura.