1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wa upinzani Kongo kufanya maandamano

24 Desemba 2023

Kundi la wagombea wa upinzani nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo wamemwandikia barua gavana wa Kinshasa kusema watafanya maandamano wiki ijayo kuhusiana na uchaguzi wa rais unaokabiliwa na utata

https://p.dw.com/p/4aWx7
Raia nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo washiriki katika zoezi la kupiga kura katika mji mkuu Kinshasa mnamo Desemba 20, 2023
Raia nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo washiriki katika zoezi la kupiga kuraPicha: Alain Uyakani/Xinhua/IMAGO

Kulingana na barua hiyo ya Desemba 22 iliyotumwa kwa gavana huyo na kuchapishwa katika mtandao wa kijamii wa X na Jean- Marc Kabunda, muakilishi wa mgombea Martin Fayulu, wagombea watano wa upinzani wanapanga maandamano ya pamoja katika mji mkuu mnamo Desemba 27.

Soma pia:Matokeo ya uchaguzi wa rais Kongo kuanza kutangazwa 

Barua hiyo imesema kuwa wataandamana kulalamika kuhusu kasoro zilizogunduliwa wakati wa shughuli ya kupiga kura na kabla ya kura hiyo.

Barua hiyo imeendelea kusema kuwa wataandamana dhidi ya kuongezwa kwa muda wa kupiga kura.

Tume ya uchaguzi CENI yakiri kuhusu ucheleweshwaji wa kura

Tume ya uchaguzi ya nchini humo, CENI imekiri kwamba kulikuwa na ucheleweshaji siku hiyo ya kura ambao unamaanisha kuwa baadhi ya vituo vilishindwa kufunguliwa, lakini imekataa madai kuwa uadilifu katika mchakato huo wa uchaguzi ulivurugwa kwa kuongeza muda wa upigaji kura.

Matokeo kamili ya awali ya uchaguzi huo yanatarajiwa kufikia Desemba 31.