1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Takriban watoto 500 wamefariki kwa njaa Sudan

Saleh Mwanamilongo
23 Agosti 2023

Shirika la misaada la Save the Children limesema takriban watoto 500 wamefariki kutokana na njaa nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4VU3J
Tschad Flüchtlinge aus Sudan Darfur
Picha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Wakiwemo watoto zaidi ya ishirini katika kituo cha watoto yatima kinachosimamiwa na serikali katika mji mkuu wa Khartoum, tangu mapigano yalipozuka nchini humo mwezi Aprili. 

Shirika la hilo pia limesema kuwa angalau watoto 31,000 wanakosa huduma ya lishe na matibabu ya utapia mlo tangu shirika hilo la misaada kusitisha shughuli zake kwenye vituo 57 vya lishe nchini Sudan.

Soma pia: Mapigano yaenea Sudan huku hofu ikizidi Darfur

Mzozo huo wa Sudan umegeuza jiji la Khartoum na maeneo mengine ya mijini kuwa viwanja vya vita. Wakazi wengi wanaishi bila maji na umeme, na mfumo wa huduma za afya nchini umekaribia kuporomoka.

Arif Noor, mkurugenzi wa shirika la Save the Children nchini Sudan amesema hawakufikiria kwamba watawaona watoto wakifa kwa njaa katika idadi na hali kama hiyo. Noor amesema wameshuhudia watoto wakifa kwa njaa inayoweza kuzuilika. Mkuu huyo wa shirika hilo la misaada amesema idadi ya watoto walioachishwa shule nchini Sudan imeongezeka pia.

''Mfumo wa elimu, sawa na sekta mbalimbali nchini, ulikuwa katika hali ngumu sana. Na kwa makadirio, kulikuwa na karibu watoto milioni saba ambao walikuwa hawako shuleni kabla ya mgogoro kuzuka na sasa idadi hii imeongezeka sana. Sasa karibu watoto milioni tisa wanahitaji msaada wa elimu. Shule nyingi zimegeuzwa kuwa kambi za wakimbizi wa ndani wengi wao wakiwa wanawake na watoto."

Visa vya utapiamlo mkali

Tschad Flüchtlinge aus Sudan Darfur
Mtoto anayeugua mtapiamlo SudanPicha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Shirika la Save the Children lilisema kati ya Mei na Julai, watoto 316 wengi wao wakiwa chini ya umri wa miaka mitano, walikufa kwa utapiamlo au magonjwa yanayohusiana katika jimbo la kusini la Nile. Zaidi ya watoto 2,400 wamelazwa hospitalini katika kipindi cha miezi minane kwa utapiamlo mkali.

Soma pia: Mzozo wa Sudan hauna dalili za kumalizika

Kwa upande wake, Mamadou Dian Balde, mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa kanda ya Afrika Mashariki na mratibu wa Sudan amesema watu 947,000 (laki tisa na arobaini elfu ) wamekimbia Sudan wakiwemo Wasudan Kusini, Waethiopia na wakimbizi wa Eritrea ambao walikuwa wametafuta makazi huko Sudan na Wasudani milioni 3.6 sasa ni wakimbizi wa ndani.

Balde alipongeza mataifa jirani ya Chad, Misri, Sudan Kusini, Ethiopia, na Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kufungua mipaka yao kwa wale wanaokimbia mapigano. Lakini alieleza wasiwasi kuhusu changamoto na vikwazo vilivyojitokeza siku za hivi karibuni katika kuwapokea wakimbizi katika nchi hizo. Pia alihimiza wafadhili kutoa kwa ukarimu msaada wa dola milioni 566 unaohitajika kwa wakimbizi wa Sudan, ambayo sasa ni asilimia 35 tu ilioyofadhiliwa.