1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaUswidi

Sweden yatangaza kisa cha kwanza cha mpox cha nje ya Afrika

15 Agosti 2024

Shirika la afya ya umma nchini Sweden limesema jana Alhamisi kwamba limerekodi kisa cha kwanza cha aina mpya kabisa ya virusi vya homa ya nyani vya clade 1b, nje ya Afrika.

https://p.dw.com/p/4jWr1
Mpox
Maambukizi ya mpox yameanza kuwa tishio ulimwenguni katika wakati ambapo tayari yametoka nje ya bara la AfrikaPicha: NIAID via AP/picture alliance

Kisa hiki cha Sweden kinatangazwa siku moja baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO kusema aina hiyo mpya ya virusi ni kiashiria tosha cha dharura ya kiafya inayoukabili ulimwengu.

Waziri wa Afya wa Sweden Jakob Forrsmed amewathibitishia waandishi wa habari kuhusiana na kisa hicho cha maambukizi ya kirusi hicho hatari kabisa cha homa ya nyani.

Soma pia:WHO: Homa ya Nyani ni dharura ya afya ya umma duniani

Mgonjwa alikwenda eneo hatarishi

Virusi aina ya clade 1b vimekuwa vikisambaa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwezi Septemba mwaka uliopita.

Mtgonjwa huyo alialiambukizwa alipokwenda barani Afrika mahali ambako kuna mlipuko mkubwa wa mpox clade 1, amesema mtaalamu wa magonjwa wa serikali ya Sweden Magnus Gisslen kwenye taarifa yake rasmi.

Amesema tayari amepata huduma na kuongeza kulingana na shirika la afya ya umma, Sweden imejiandaa kuchunguza, kuwatenga na kuwatibu watu walioambukuizwa mpox kwa kuzingatia usalama.

Ujerumani | Chanjo ya Mpox-(2022)
Chanjo za virusi vya mpox zinapatikana, ingawa hazina uwezo wa kudhibiti aina zote za virusi hivyoPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Mpox ni nini?

Mpox kwa mara ya kwanza iligunduliwa kwa binaadamu miaka ya 1970, katika eneo ambalo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ugonjwa huo uligundulika kwanza kwa nyani na kutambulika kama homa ya nyani.

Maambukizi husababisha homa, maumivu ya misuli na mapele makubwa kwenye ngozi. Chanjo ya virusi hivyo inapatikana, lakini yenye uwezo wa kudhibiti aina fulani tu ya virusi.

Soma pia: Hofu yatanda kufuatia mlipuko mpya wa homa ya nyani

Virusi hivyo huambukizwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binaadamu, lakini pia vinaweza kusambaa miongoni mwa binaadamu ikiwa watagusana na mtu aliyeambukizwa.

Shirika la WHO siku ya Jumatano lilitangaza mlipuko wa homa ya nyani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mataifa jirani kama dharura ya kiafya ulimwenguni.

Hii ni mara ya pili kwa WHO kuchukua hatua hiyo katikati ya mlipuko wa maradhi hayo, baada ya mwaka 2022, kutangaza kama wasiwasi wa kiafya ulimwenguni.