1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Homa ya Nyani ni dharura ya afya ya umma duniani

15 Agosti 2024

Mkurugenzi wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameitangaza Mpox kuwa ni dharura ya afya ya umma duniani kutokana na kuongezeka kwa maambukizi yake barani Afrika.

https://p.dw.com/p/4jURS
WHO-Chef Tedros Ghebreyesus
Picha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

Mkurugenzi wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ametangaza hatua hiyo baada ya mkutano na kamati ya dharura ya shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa.

WHO, imesema zaidi ya watu 14,000 wameambukizwa virusi vya mpox hadi sasa katika mwaka huu huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wengine wapatao 524 wameshakufa.

Tedros Adhanom Ghebreyesus | Mkurugenzi, WHO
Mkurugenzi wa WHO, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Shirika la Afya la Umoja wa Afrika lilitangaza hali ya dharura ya afya ya umma siku ya Jumanne kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo wa Homa ya Nyani unaoongezeka katika bara hilo, likisema hatua hiyo ni wito wa wazi kwa mamlaka zote kuchukua hatua.

Soma Pia: Africa CDC yatangaza dharura ya kiafya kutokana na homa ya nyani Afrika 

Mkuu wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika, CDC, Jean Kaseya ameeleza kuwa kirusi cha Mpox kwa sasa kimevuka mipaka katika kusambaa kwake na kimewaathiri maelfu ya watu katika bara la Afrika. Wanasayansipia wameelezea wasiwasi wao juu ya kuenea kwa aina mpya ya ugonjwa ambao watu wanaweza kuambukizana kirahisi.

DRC | Homa ya Nyani
Familia ya Beyande Kidicho ambayo watoto wake walipata maambukizi ya Homa ya Nyani. Picha ilipigwa tarehe Oktoba 4, 2022.Picha: Arlette Bashizi /REUTERS

Kituo cha CDC barani Afrika, kimeripoti kwamba kirusi cha mpox sasa kimegunduliwa katika nchi takribani 13 za Afrika. Shirika hilola afya la Umoja wa Afrika limesema maambukizi yameongezeka kwa asilimia 160 na idadi ya vifo pia imeongezeka kwa asilimia 19.

Soma Pia:  CDC-Afrika yaelezea matumaini ya kufikishwa chanjo ya Mpox, barani Afrika  

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limesema homa ya nyani iligundulika hivi karibuni kwa mara ya kwanza katika nchi nne za Afrika Mashariki ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda. Gebreyesus amesema kuna wasiwasi wa kuenea zaidi kwa maambukizi ya mpox barani Afrika na kwingineko duniani.

Vyanzo: AP/AFP