Stoltenberg aonya dhidi ya kuigawa Marekani na Ulaya
15 Februari 2024Huku wakikabiliwa na vita vya Ukraine ambavyo vimesababisha shinikizo kubwa kwa raslimali za kijeshi na fedha, na msaada wa Marekani ukikabiliwa na mvutano katika bunge la Marekani, viongozi wa Ulaya na maafisa wa vyeo vya juu wametahadharisha kwamba Ulaya sharti iwekeze zaidi katika majeshi yake na teknolojia mpya, na kuongeza utengenezaji wa silaha.
Akizungumza na waandishi habari mjini Brussels, Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, amesema anakaribisha hatua ya washirika wa Ulaya kuwekeza zaidi katika masuala ya ulinzi na NATO imekuwa ikitaka hivyo kwa miaka mingi.
"Umoja wa Ulaya wanawekeza zaidi katika ulinzi na NATO imetaka hivyo kwa miaka mingi. NATO imewataka washirika wa Ulaya wawekeze fedha nyingi zaidi kadri inavyowezekana, wawe na vikosi zaidi, wawe tayari kukabiliana na kitisho na washirika wa Ulaya wanatimiza maagizo haya. Hilo ni jambo jema, lakini sio mbadala kwa NATO, bali ni njia ya kuiimarisha NATO."
Kauli ya Trump yakosolewa
Stoltenberg aliongeza kusema, "Hatutakiwi kuchukua mkondo unaoashiria wanajaribu kuitenga Ulaya na Amerika Kaskazini. Nguvu ni kuwa na Ulaya na Amerika Kaskazini pamoja.. ndani ya NATO."
Jumamosi iliyopita rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alisema aliwahi kutahadharisha atairuhusu Urusi ifanye chochote inachokitaka kwa wanachama wa NATO ambao hawatengi kiwango cha asilimia 2 cha pato jumla la taifa kwa ajili ya ulinzi.
Rais wa Marekani Joe Biden aliyaeleza matamshi ya Trump kuwa ya hatari, yasiyoiwakilisha Marekani na yanayochochea hali wa mashaka miongoni mwa washirika wa Marekani kuhusu uwezo wake wa kutegemewa katika ngazi ya kimataifa siku za usoni.
Soma pia: Umoja wa Ulaya walaani kitisho cha Trump kwa NATO
Stoltenberg amesema kauli za Trump zinaibua maswali kuhusu uhalali wa jukumu la pamoja la usalama la NATO katika ibara ya tano ya mkataba ulioiasisi jumuiya hiyo, inayosema kwamba shambulizi kwa nchi yoyote mwanachama litajibiwa na nchi zote wanachama.
Stoltenberg aidha amesema uwezo wa NATO kuzuia mashambulizi unategemea kwa sehemu silaha za nyuklia za Marekani zilizopo barani Ulaya zinazotumia miundombinu ya Ulaya. Nchi kadhaa wanachama wa NATO zinachangia ndege kutumika katika jukumu la nyuklia, pamoja na maafisa waliopewa mafunzo, lakini Marekani inashikilia udhibiti kamili wa matumizi ya silaha hizo.
(ap)