Umoja wa Ulaya walaani kitisho cha Trump kwa NATO
12 Februari 2024Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel amekiita kitishio cha Rais wa Zamani wa Marekani Donald Trump kwamba endapo atakachuguliwa tena kuwa rais hatozilinda nchi za Jumuiya ya NATO ambazo hazitowajibika vyema katika uchangiaji wa jumuiya hiyo kuwa ni uzembe. Kupitia ukurawa wake wa X, zamani Twitter, Michel amesema kwa takribani miaka 75 jumuiya hiyo imekuwa na jukumu la kuimarisha usalama na ustawi wa Wamarekani, watu wa Ulaya hadi Canada kwa kipindi chote hicho.Aidha ameongeza kwa kusisitiza tena uhitaji wa Ulaya kuendelea kwa kasi zaidi katika mkakati na kuwekeza katika ulinzi wake. Jumamosi iliyopita Trump alitoa kitisho cha kwamba iwapo atachaguliwa tena nchini Marekani, hatawatetea wanachama wa NATO ambao hawajatimiza wajibu wao wa kifedha, na kwenda umbali zaidi kwa kutoa kauli iliyoonesha kama akihimiza Urusi kuwashambulia.