Bunge Pakistan lamchagua Sharif baada ya kumuondoa Khan
11 Aprili 2022Kuchaguliwa kwa Sharif kunahitimisha mzozo wa kikatiba uliodumu kwa wiki nzima ambao ulifikia kilele siku ya Jumapili wakati Khan alipopoteza kura ya kutokuwa na imani naye, ingawa taifa hilo linalomiliki silaha za nyuklia huenda likaendelea kukabiliwa na misukosuko ya kisiasa na kiuchumi.
Soma pia: Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan aondolewa madarakani
Sharif, mwenye umri wa miaka 70, ambaye anasifika ndani ya nchi kuwa msimamizi mzuri zaidi kuliko mwanasiasa, ni mdogo wake Nawaz Sharif, alieshika nafasi ya waziri mkuu mara tatu.
Wachambuzi wanasema Shehbaz, tofauti na Nawaz, ana uhusiano mzuri na jeshi la Pakistan, ambalo kijadi linadhibiti sera za kigeni na ulinzi katika nchi hiyo yenye watu milioni 220.
Baada ya kura hiyo, Sharif ameapa kukabiliana na hali mbaya ya kiuchumi ambayo imesababisha sarafu ya Rupia kushuka zaidi na benki kuu kupandisha riba kwa kiwango chake kikubwa zaidi katika miongo wiki iliyopita.
Chama cha Khan chajitoa bungeni
Dakika chache kabla ya kura y akumchagua waziri mkuu, wabunge wa chama cha Khan walijiuzulu kwa wingi kutoka katika baraza la chini la bunge kupinga uundwaji wa serikali uliotarajiwa na mahasimu wake wa kisiasa.
Soma pia: Waziri Mkuu wa Pakistan akabiliwa na kura ngumu ya kutokuwa na imani naye
Shah Mahmood Qureshi, waziri wa zamani wa mambo ya nje na makamu wa rais wa chama cha Khan, aliliambia baraza hilo kuwa wabunge wao wote wanajiuzulu ubunge.
"Kwa mashauriano ya kiongozi wetu Imran Khan, sisi wa chama cha Tehreek-e-Insaf tumeamua kutoshiriki katika mchakato huu wa uchaguzi usio na msingi, na tunatangaza kujiuzulu ubunge."
Chama cha Khan Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) kilikuwa kimewasilisha nyaraka za kumteua Qureshi kama mgombea wake wa nafasi ya waziri mkuu.
Sharif mdogoaliibuka kuwa kiongozi wa upinzani ulioungana kumpindua Khan, nyota wa zamani wa kriketi ambaye amedai kuwa Marekani ndiyo iliyosababisha anguko lake, jambo ambalo Washington imekanusha.
Soma pia: Wabunge Pakistan kuanza kupiga kura ya kutokuwa na imani na Khan
Mara baada ya kuchaguliwa, Sharif ametangaza hatua kadhaa za kutafuta umaarufu, zikijumuisha mshahara mpya wa kima cha chini wa zaidi wa rupia 25,000, sawa na karibu dola 135, nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma, na miradi ya maendeleo katika maeneo ya mashambani.
Mara baada ya kuapishwa, kazi ya kwanza ya Sharif itakuwa kuunda baraza la mawaziri ambalo pia litakuwa na wajumbe wengi kutoka kwa chama cha mrengo wa kati-kushoto cha Pakistan Peoples Party (PPP), na pia kutoa nafasi kwa kundi dogo la kihafidhina la Jamiat-ulema-e-Islam.
Chanzo: Mashirika