Wabunge Pakistan kupiga kura ya kutokuwa na imani na Khan
31 Machi 2022Bunge la Pakistan linajiandaa kupiga kura ambayo itaamua hatima ya waziri mkuu Imran Khan,kura ya ama kuwa na imani nae au ya kutokuwa na imani nae na pengine kusababisha kuondolewa madarakani mwanasiasa huyo na kushuhudia Pakistan ikirudi tena kwenye mashaka ya kisiasa.
Imran Khan mwenye umri wa miaka 69 anakabiliwa na hali ngumu ya kukosolewa iliyoongezeka kutokana na utendaji kazi wake ikiwemo lawama za kusimamia vibaya uchumi wa taifa hilo ambalo linakabiliwa na mfumko mkubwa wa bei na kupanda kwa nakisi ya bajeti. Jana Jumatano Khan alipoteza uungwaji mkono bungeni baada ya chama mshirika wake mkuu kwenye serikali yake ya muungano kujiondowa serikalini.
Kiongozi wa upinzani Bilawal Bhutto Zardari ansema Khan hana namna ya kujinasua.
Kiongozi wa chama cha upinzani Bilawal Bhutto Zardari ambaye ni mwanawe wa kiume aliyewahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo,aliyeuwawa Benazir Bhutto amewaambia waandishi wa habari bungeni wampelekee ujumbe Imran Khan kwamba hakuna namna rahisi ya kujinusuru lakini fikra pekee anayoweza kumwambia ni kuondoka mwenyewe kwa heshima.
Hii leo Imran Khan anasubiriwa kulihutubia taifa wakati wabunge wakijiandaa jumapili kupiga kura ya ama kumuondowa madarakani au kumuacha.
Gazeti la Pakistan lahitimisha kuondoka kwa Khan.
Tayari lakini gazeti maarufu sana nchini Pakistan linaloandika kwa lugha ya kingereza-Dawn limeandika kwenye sehemu ya uhariri wake katika ukurasa wake wa mwanzo wa chapisho la kwenye mtandao hii leo kwamba waziri mkuu kimsingi ameshaporomoka. Na hasa baada ya hapo jana chama mshirika wake mkuu bungeni cha Vuguvugu la Qaumi MQM kujiondowa kwenye muungano unaotawala na kujielekeza katika kambi ya upinzani inayopania kumtimua.
Viongozi wa upinzani walimtaka waziri mkuu huyo ajiuzulu hata kabla ya kupoteza wingi bungeni lakini wasaidizi wake walisema hana mpango huo. Pamoja na yote hayo kuondolewa madarakani Imran Khan kunaweza kumaanisha Pakistan inaingia kwenye duru nyingine ya ukosefu wa utulivu,nchi ambayo jeshi kwa muda mrefu linahistoria ya kujiingiza kwenye siasa na hakuna waziri mkuu aliyewahi hata mara moja kukamilisha muhula mzima wa miaka mitano.
Mwandishi.Saumu Mwasimba.
Mhariri: Zainab Aziz