1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Pakistan yamvua madaraka waziri mkuu Sharif

28 Julai 2017

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif amejiuzulu wadhifa wake kufuatia agizo la mahakama ya juu zaidi nchini humo la kutaka kuondolewa kwa kiongozi huyo kutokana na mashtaka ya rushwa yanayomkabili.

https://p.dw.com/p/2hIhB
Pakistan Premierminister Nawaz Sharif
Mwisho wa enzi? Waziri Mkuu Nawazi Sharif amepoteza tena kiti chake kwa mara ya pili.Picha: Reuters/C. Firouz

Mahakama hiyo ya juu zaidi nchini Pakistan leo hii iliamua kumvua madaraka Waziri mkuu Nawaz Sharif kufuatia uchunguzi wa kashfa ya rushwa kuhusiana na utajiri wa familia yake, hatua ambayo imeufikisha kikomo muhula wake wa tatu akiwa madarakani na kuagiza uchunguzi wa jinai kufanyika dhidi ya familia yake.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa, mahakama hiyo pia imemuondoa mamlakani waziri wa fedha Ishaq Dar ambaye ni mmoja wa washirika wa karibu zaidi ambaye alisifika sana kwa kuongeza kiwango cha kasi ya ukuaji wa uchumi katika kipindi cha muongo mmoja. 

Pakistan Islamabad Urteil Korruptiosnprozess
Askari polisi wa Pakistan wakilinda usalama mbele ya jengo la mahakama ya juu kabisaa nchini humo wakati wa kesi dhidi ya waziri mkuu Sharif ikiendelea kusiikilizwa.Picha: Getty Images/AFP/A. Qureshi

Waziri mkuu Nawaz Sharif, baada ya kuhojiwa na timu ya pamoja ya uchunguzi kwenye jengo la mahakama, kuhusiana na madai ya kuwa na makampuni ya familia yake nje ya nchi, alisema kilichotokea siyo rushwa wala matumizi mabaya ya madaraka, lakini masuala binafsi kugeuzwa ya kisiasa.

Chama tawala kinachoongozwa na Sharif cha Muslim League-Nawaz, PML-N, ambacho pia kina idadi kubwa ya wabunge kinatarajia kumtaja waziri Mkuu mpya atakayeshika wadhifa huo hadi hapo uchaguzi mkuu utakapofanyika mwakani.

Mahakama hiyo ya juu kwa kauli moja imeamua kwamba Sharif hakufaa kuendelea kusalia madarakani baada ya jopo la uchunguzi kudai kuwa familia yake haingeweza kuthibitisha namna ilivyopata mali hiyo nyingi.

Kabla ya maamuzi hayo, baadhi ya mawaziri, ambao ni pamoja na washirika wa karibu sana wa Sharif walisema chama tawala kitaheshimu maamuzi ya mahakama hiyo ya juu.

Wachambuzi wanaonya kuhusu kuibuka kwa mzozo mwingine wa kisiasa unaoweza kufifisha uwezekano wa wawekezaji wa kigeni, ambao walikuwa wakifikiria kuwekeza nchini humo, ambao wanaweza kutishiwa kwa kutokuwepo kwa usalama na mazingira magumu ya biashara.

Pakistan Finanzminister Ishaq Dar
Waziri wa fedha Ishaq Dar ambaye pia amevuliwa wadhifa wake katika uchunguzi wa rushwa uliokuwa unafanyika dhidi ya familia ya waziri mkuu Sharif.Picha: Getty Images/AFP/A. Qureshi

Mapema kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo na mahakama, uliomtia hatiani Waziri mkuu huyo, mmoja wa viongozi wastaafu wa serikali Nasir Khan alisema Nawaz Sharif ndiye mfanyabiashara pekee aliyefanya mengi nchini Pakistan. 

Awamu mbili za awali za utawala wa Sharif pia zilikatizwa, kwa mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1999, lakini alirejea kutoka uhamishoni na kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2013.

Mwandishi: Lilian Mtono

Mhariri: Josephat Charo