Sekretarieti ya EAC yawasilisha makadirio ya bajeti yake
14 Juni 2023Katika hotuba yake ya uwasilishwaji wa bajeti, mwenyekiti wa mawaziri wa jumuiya hiyo Ezechiel Nibigira raia wa Burundi, amebainisha kwamba makadirio ya bajeti ya mwaka huu yanawasilishwa wakati uchumi wa jumuiya hiyo kongwe barani Afrika, ukiwa mashakani kutokana na misukosuko ya kimataifa ikiwapo vita na mabadiliko ya tabia nchi.
Hotuba hiyo iliyosomwa katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki Arusha Tanzania pia ilibainisha kwamba pamoja na changamoto hizo, lakini ukuaji wa uchumi katika ukanda huo uliimarika kwa asilimia 4. 8 mwaka 2022, kutoka asilimia 3.5 mwaka 2021.
Bajeti hiyo imezingatia maeneo tisa ya vipaumbele, ikiwapo uimarishaji wa michakato ya utawala wa kikanda, uboreshaji wa mifumo ya forodha pamoja na usimamizi wa mifumo ya amani ya kikanda na kimataifa.