Mawaziri wa ulinzi wa EAC wajadili usalama wa Kongo
29 Mei 2023Ripoti hiyo ya wakuu wa majeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki inaonesha kuwa bado kuna changamoto tele mashariki mwa Kongo zinazotatiza mchakato wa amani na usalama katika eneo hilo.
Waziri wa Ulinzi wa Burundi, Alain Tribert Mutabazi, amesema licha ya kuwepo kwa majeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliokwenda kuhakikisha amani inarejea, bado eneo hilo la Kongo limesalia kuwa uwanja wa mapigano.
"Mashambulizi ya makundi ya wapiganaji wa ADF, wale wa M23, Red Tabara yamekuwa yakiwauwa raia na kupelekea wengine maelfu kadhaa kuyakimbia makaazi yao. Licha ya majeshi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwepo hapo, changamoto bado ni nyingi na safari imesalia ndefu. Ndio sababu tunakutana hapa ili tuwaandaliye marais wetu ripoti ya makadirio ya hali ilivyo na hatua ilopigwa, kwani hali ya usalama haujaimarika, na juhudi zaidi zinahitajika."
Marais wa nchi wanachama kukutana Bujumbura
Hata hivyo, waziri huyo amesema kuwa ripoti ya wakuu wa majeshi imetowa mapendekezo ambayo kama yatatekelezwa basi hali ya usalama inaweza kuimarika mashariki mwa Kongo.
Baada ya kutathminiwa na mawaziri hao wa ulinzi, ripoti hiyo ya wakuu wa majeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki itakabidhiwa kwa marais ambao watakutana hapa mjini Bujumbura Jumatano wiki hii.
Wakati Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alipokuja Bujumbura katika juhudi za kurejesha amani mashariki mwa Kongo, alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inapendelea kuona amani na usalama uliopo Burundi unapatikana pia Kongo.
Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika, Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi, amekuwa akiongoza juhudi za kuhakikisha usalama unapatikana mashariki mwa Kongo, ambapo mwezi uliopita, marais kutoka nchi 13 zinazopakana na Maziwa Makuu walikutana mjini Bujumbura, katika mkutano ulohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.