Scholz: Ujerumani itawekeza zaidi katika sekta ya ulinzi
10 Novemba 2023Scholz amesema kitita maalum cha dola bilioni 107 kwa Jeshi la ulinzi la Shirikisho "Bundeswehr" ni hatua ya kwanza muhimu, lakini ameahidi kuwa mwaka ujao, Ujerumani itafikia uwekezaji wa kiwango cha asilimia mbili cha pato ya ghafi la taifa katika sekta ya ulinzi.
Akihutubia mkutano wa Jeshi la Ulinzi la Ujerumani, Bundeswehr, Scholz amezungumzia mfuko maalum wa serikali ulioanzishwa ili kufufua uwezo wa jeshi baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Vita hivyo vilivyoanza Februari mwaka jana, viliibua maswali juu ya utayari wa jeshi la Ujerumani na kuzilazimisha serikali za mataifa ya Ulaya kutathmini upya mikakati yao ya ulinzi.
Scholz amethibitisha kuwa Ujerumani itatumia 2% ya pato ghafi la taifa katika sekta ya ulinzi kama ilivyotajwa kwenye malengo ya Jumuiya ya Kujihami NATO, na kusema kwa mara ya kwanza Ujerumani itatimiza urari huo mwaka ujao.
Soma pia:Ujerumani kuipa NATO wanajeshi 35,000 kuanzia 2025
Ili kufikia azma hiyo, serikali mjini Berlin italazimika kutumia zaidi ya euro bilioni 20 kila mwaka katika sekta ya ulinzi. Kansela huyo wa Ujerumani amesema azma hiyo itakuwa ya muda mrefu na akaikadiria kuwa ni ndani ya kipindi kilichosalia cha miaka ya 2020 na kile cha kuanzia miaka ya 2030. Aidha Scholz ameelezea ni kwanini Ujerumani imechukua uamuzi huu:
" Ingawa ni ngumu kuafiki, kwa sasa hatuishi katika nyakati za amani duniani. Mfumo wetu wa amani uko hatarini. Lakini tumethibitisha kuwa tunaweza kupiga hatua licha ya changamoto. Leo hii, hakuna anayeweza kutilia shaka kile ambacho hapa Ujerumani tumekuwa tukijaribu kukiepuka kwa muda mrefu, nacho ni kwamba tunahitaji "Bundeswehr" yenye nguvu. Tunahitaji jeshi lenye uwezo wa kuilinda nchi yetu. Tunahitaji nyenzo na vikosi vilivyo tayari na vyenye uwezo wa kulinda usalama wa eneo la pamoja na washirika wetu popote pale vitakapohitajika."
Hatua nyingine za Ujerumani katika sekta ya ulinzi
Mbali na ufadhili huo, Scholz amesema hatua nyingine kuu itakayofuatia mabadiliko hayo, itakuwa kupambana na vikwazo vya urasimu na kiutendaji ambavyo amesema kwa miaka mingi vimekuwa vikipunguza kasi ya askari wa Ujerumani.
Ameendelea kusema kwamba hali ya kisiasa duniani inathibitisha bila shaka umuhimu wa mabadiliko haya ya sera, hasa akielezea uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na mashambulizi ya kikatili yaliyoendeshwa mwezi uliopita nchini Israel na kundi la Hamas na kuzusha vita katika eneo la Mashariki ya Kati.
Soma pia: Ujerumani: NATO yapaswa kujiimarisha kufuatia vita Ukraine
Serikali ya Scholz itajadili pamoja na viongozi wa Bundeswehr katika siku zijazo kuhusu mustakabali wa jeshi hilo pamoja na kuanzisha mpangilio mpya wa Wizara ya Ulinzi. Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa itakuwa ni pamoja na suala lililo mezani la kupelekwa kikosi maalum nchini Lithuania.
Haya yanajiri siku moja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius kuwasilisha miongozo yake mpya ya sera ya ulinzi, ambayo inafafanua masuala ya ulinzi wa kitaifa na ule wa kiushirika kuwa jukumu kuu na kuangazia kwamba uwezo wa vita ndiyo kanuni muhimu.
(Chanzo: DPAE)