Scholz azungumza na China kutumia ushawishi wake kwa Urusi
20 Juni 2023Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema amezungumza na waziri mkuu wa China Li Qiang kuhusu jinsi ya kutumia ushawishi wake dhidi ya Urusi kuvifikisha mwisho vita nchini Ukraine.
Akizungumza baada ya mkutano kati ya serikali ya Ujerumani na China mjini Berlin Jumanne Sholz amesema ni dhahiri wanapitia kipindi cha changamoto katika siasa za dunia ambazo pia zinaathiri biashara ya kimataifa na mahusiano ya kiuchumi.
"Itakuwa rahisi kwa kila nchi ulimwenguni kuyafikia malengo yake ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa tutaruhusu ushindani wa haki, uwazi katika kuyafikia masoko na usawa wa kufanya biashara. Ushindani huimarisha uvumbuzi. Sote tunapiga hatua haraka kupitia mabadiliko tunapobadilishana teknolojia bila uoga wa kupuuzwa kwa haki miliki.'', alisema Scholz.
Kansela Scholz amesisitiza kwamba serikali yake imejitolea kwa dhati kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na China na kuongeza kuwa kulifikia soko la China pamoja na hali ya kampuni za Ujerumani na nchi za kigeni bado ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa kwa dhati ili kuboresha.
Kansela Scholz pia amesisitiza umuhimu wa haki za binadamu katika uzalishaji wa bihaa za viwandani na mnyororo wa ugavi wa bidhaa.