Waziri Mkuu wa China ziarani katika mataifa mawili ya Ulaya
19 Juni 2023Li, ambaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa China mnamo mwezi Machi, ameanza ziara yake katika nchi nchi mbili ambapo pia atatembelea Ufaransakwa ajili ya mkutano wa kilele wa ufadhili wa mazingira ulioandaliwa na Rais Emmanuel Macron. Waziri Mkuu Li, ambaye hii ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu aingie madarakani, alipokelewa na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier mapema siku ya Jumatatu.
Rais Steinmeier amesisitiza juu ya umuhimu wa uhusiano baina ya China na Marekani kwa ajili ya "usalama na ushirikiano wa kimataifa". Kulingana na ujumbe uliochapishwa na msemaji wa ofisi ya Rais wa Ujeumani Cerstin Gammelin, kupitia ukurasa wa Twitter, Rais Steinmeier amezihimiza Beijing na Washington kuimarisha njia za mawasiliano baina yake, huku pia akiitaka China kutumia "mizani yake ya kisiasa na ushawishi kwa Urusi ili kuleta amani" nchini Ukraine. Ziara ya waziri mkuu wa China Li, nchini Ujerumani na Ufaransa inafanyika wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken naye akikamilisha ziara ya juu mjini Beijing, ambako kumekuwa na ishara ya matumaini baada ya Rais wa China Xi Jinping aliyekutana na Blinken kusema kwamba kumekuwa na "maendeleo fulani".
Li na ujumbe wake mkubwa wa mawaziri wa China utakutana na Kansela Olaf Scholz na wenzao wa Ujerumani siku ya Jumanne, ikiwa ni mara ya saba kwa wawakilishi wa nchi hizo mbili kufanya mazungumzo ya kiserikali. Maafisa wakuu kutoka pande zote mbili pia watakutana na wawakilishi wa biashara.
Lakini hata hivyo, mkakati wa usalama wa kitaifa wa Ujerumani uliowasilishwa siku chache zilizopita unaweza kutoa mwelekeo wa jinsi mazungumzo hayo yatakavyokuwa. Mkakati huo uliishutumu vikali China kwa kwenda kinyume na maslahi ya Ujerumani, kuweka usalama wa kimataifa "chini ya shinikizo kubwa" na kudharau haki za binadamu. Wakati huohuo ulisisitiza umuhimu wa kupata ushirikiano wa China katika masuala ya kimataifa kama vile kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Kansela Scholz mwenyewe alisema ujumbe uliotolewa na mkakati huo ni kwamba "ushirikiano wa China katika biashara ya dunia na uhusiano wa kiuchumi wa dunia haupaswi kuharibika. Lakini wakati huohuo masuala ya kiusalama yanayoibuka kati yetu yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito".
China imekuwa ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Ujerumani katika miaka ya hivi karibuni, ingawa ilikuwa tu mbele kidogo ya Marekani katika robo ya kwanza ya mwaka huu. Kansela Scholz alitembelea China mnamo mwezi Novemba kukutana na Xi, aliyeonya dhidi ya matumizi ya vitisho au matumizi ya silaha za nyuklia.