Rais Xi, Kansela Scholz watafuta kuimarisha ushirikiano
4 Novemba 2022Scholz ndiye kiongozi wa kwanza la taifa la G7 kuzuru China tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona, lililopelekea taifa hilo la pili kiuchumi duniani kufunga mipaka yake na Rais Xi Jinpingkuepuka kwa kiasi kikubwa diplomasia binafsi.
Ziara hiyo ya kansela wa Ujerumani, ambaye ameambatana na watendaji wa juu wa sekta ya biashara, imezua utata nuymbani, ikija mara tu baada ya Xi kuimarisha udhibiti wake madarakani.
Mzozo unafukuta pia kati ya mataifa ya magharibi na Beijing kuhusiana na masuala kadhaa kuanzia Taiwan hadi madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Soma pia: Uhusiano baina ya Ujerumani na China watimiza miaka 50 ukilegalega
Kansela Scholz, aliepokelewa na Xi katika Jumba la Ukumbi wa Watu la mjini Beijing baada ya kuwasili, amesema anatumai kuendeleza zaidi ushirikiano wa kiuchumi, huku akigusia pia maeneo yanayozusha tofauti.
"Ni vyema kwamba tunaweza kuzungumza hapa kuhusu masuala yote, yakiwemo yale ambako tuna mitazamo tofauti. Hiyo ndiyo shabaha ya mazungumzo, na ninafurahi kwamba hili linawezekana kwa pamoja leo," alisema Scholz.
Umuhimu kwa China na Ujerumani kushirikiana zaidi
Shirika la habari la China Xinhua limesema Xi ametilia mkazo haja ya China na Ujerumani, madola makubwa mawili yenye ushawishi mkubwa, kushirikiana pamoja katika nyakati za mabadiliko na ukosefu wa utulivu, na kuchangia zaidi katika amani ya dunia na maendeleo.
Scholz pia maezungumza na waziri mkuu wa China Li Kenqiang, aktika mkutano ambamo ametoa wito wa biashara ya usawa kati ya mataifa hayo mawili.
Soma pia: Merkel aitaka China kuzungumzia haki za binaadamu
Ujumbe wa zaidi ya watu 60 ulipokelewa katika uwanja wa ndege wa Beijing na kikosi cha ulinzi wa kijeshi pamoja na wafanyakazi wa afya waliofanya vipimo vya laazima vya corona katika mabasi yaliogeuzwa maabara zinazotembea.
Kulingana na serikali ya Ujerumani, kipimo cha Scholz kilifanywa na daktari wa Kijerumani alieambatana naye na kusimamiwa na maafisa wa afya wa China.
Wasiwasi wa kuitegema zaidi China
Umuhimu wa kiuchumi wa China unatazamwa na baadhi mjini Berlin kuwa wa maana sana kuliko wakati wowote, wakati ambapo Ujerumani inakabiliwa na kitisho cha kutumbukia katika mdororo, ikikabiliwa na mzozo wa nishati uliosababishwa na vita nchini Ukraine.
Soma pia: Rais Vladimir Putin ayasifia mahusiano yake na Xi Jinping
China ni soko kubwa kwa bidhaa za Ujerumani, kuanzia mashine hadi magari yanayotengenezwa na kampuni kama Volkswagen, BMW na Mercedes-Benz.
Lakini utegemezi mkubwa wa viwanda vya Ujerumani kwa China, unakabiliwa na uchunguzi, baada ya utegemezi uliopitiliza kwa nishati ya Urusi kuiacha katika hatari wakati Moscow ilipoamua kuzima mabomba yake.
Chanzo: Mashirika