SANTIAGO : Ghasia zaandama kifo cha Pinochet
11 Desemba 2006Polisi wa kutuliza ghasia wamepambana na maelfu ya waandamanaji nchini Chile kufuatia kifo cha dikteta wa zamani wa nchi hiyo Augusta Pinochet hapo jana.
Msemaji wa polisi amesema polisi 23 wamejeruhiwa katika ghasia hizo.Mamia waliteremka mitaani kusheherekea kifo cha Pinochet karibu na Kasri la Rais katika mji mkuu wa Santiago. Rais Michelle Bachelet amesema hakutakuwepo na mazishi ya kitaifa au ombolezo la kitaifa kwa rais huyo wa zamani.Bachelet na wazazi wake waliwahi kutiwa mahabusu wakati wa utawala wa Pinochet ulioanzia mwaka 1973 na kuishia mwaka 1990.
Pinochet anashutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu za madarzeni ya watu lakini hakuwahi kusimama kizimbani kujibu mashtaka kutokana na afya yake kuwa mbaya.Takriban watu 3,000 kwa mujibu wa takwimu rasmi waliuwawa au kuteswa wakati wa utawala wa Pinochet.
Pinochet anatarajiwa kuzikwa hapo Jumanne kwa heshima za kijeshi.