Salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Berlusconi
12 Juni 2023Berlusconi aliyekuwa na ushawishi mkubwa, alikabiliwa na matatizo ya kiafya kwa miaka kadhaa, huku akifanyiwa upasuaji wa moyo mnamo mwaka 2016 na kulazwa hospitalini mwaka 2020 baada ya kupata maambukizi ya Covid-19. Licha ya kuchaguliwa tena kuwa Seneta mwaka jana, alionekana kwa nadra hadharani.
Toka kutangazwa kifo chake, salamu za rambirambi zimetolewa na viongozi mbalimbali ulimwenguni. Kuanzia nyanja ya kisiasa, kiuchumi hadi madawati ya michezo. Waziri Mskuu wa Italia, Georgia Meloni, amesema Berlusconi alikuwa mpambanaji asiyeogopa kutetea kile anachokiamini.
''Alikuwa rafiki mkubwa wa Urusi''
Matteo Salvini, mkuu wa muungano wa vyama vinavyopinga uhamiaji nchini Italia alisema nchi hiyo imempoteza Muitaliano mkubwa. Naye Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema kifo cha Berlusconi ni hasara kwa siasa za dunia.
"Bila shaka, alikuwa mwanasiasa wa Ulaya na tunaweza kusema na wa kiwango cha kimataifa. Hakuna watu wengi kama hao katika uwanja wa siasa za kimataifa hivi sasa. Alikuwa rafiki mkubwa wa Urusi na alifanya mengi kukuza biashara na uhusiano wa kirafiki kati ya Urusi na nchi za Ulaya.'', alisema Putin.
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban alisema kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba mwendazake alikuwa mpambanaji mkuu.
Katika ujumbe kwa binti mkubwa wa Berlusconi, Marina, Papa Francis alihakikisha ushiriki wake wa dhati katika maombolezo ya kupoteza mhusika mkuu wa maisha ya kisiasa ya Italia.
Mazishi ya kitaifa mjini Milan
AC Milan, klabu ya soka ambayo ilishinda mataji mengi ya ndani na Ulaya chini ya umiliki wa Silvio Berlusconi, ilimwita kiongozi huyo kuwa ni mtu asiyesahaulika.
Berlusconi aliingia ofisini kwa mara ya kwanza mwaka wa 1994 na aliongoza serikali nne hadi 2011. Uongozi wake kama Waziri Mkuu wa Italia ulikumbwa na kashfa chungu nzima za ngono na tuhuma za ufisadi ambazo alifanikiwa kujinasua.
Silvio Berlusconi, alizaliwa mwaka wa 1936 huko Milan, Berlusconi alianza kazi yake ya kuuza vifaa vya usafi, kabla ya kuanzisha kampuni ya ujenzi. Aliendelea kuwa mmoja wa watu tajiri zaidi wa Italia, akitengeneza utajiri wake kupitia chaneli zake za televisheni. Berlusconi, alipata kutambuliwa kimataifa kama mmiliki wa klabu maarufu ya soka ya AC Milan ambayo aliiokoa kutokana na kufilisika mwaka 1986 kabla ya kuingia kwenye siasa.
Mazishi ya kitaifa ya Silvio Berlusconi yatafanyika Jumatano Juni 14 kwenye kanisa kuu la mji wa Milan.