1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlusconi akanusha kula njama kumuangusha Draghi

22 Julai 2022

Waziri mkuu wa zamani, Silvio Berlusconi, amekanusha kuwa chama chake kilikula njama yoyote ya kuiangusha serikali ya waziri mkuu wa sasa na ambaye amejiuzulu kwa mara ya pili ndani ya wiki moja, Mario Draghi.

https://p.dw.com/p/4EVeC
Italien Silvio Berlusconi AC Monza
Picha: Italy Photo Press Worldwide/picture alliance

Berlusconi, ambaye chama chake cha Forza Italia kinachofuata siasa za mrengo wa kati kulia na kile cha mrengo wa kulia League vilikataa kupiga kura ya imani, na hivyo kumlazimisha Draghi kujiuzulu, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa (Julai 22) kwamba Draghi hakulazimika kujiuzulu na badala yake angelichukuwa uamuzi mwengine.

Waziri mkuu huyo wa zamani ambaye bado anatajwa kuwa na nguvu miongoni mwa wapigakura alisema yeye na chama chake hawahusiki na kuporomoka kwa Draghi.

"Yaliyojiri si kola letu hata kidogo. Tulimuambia Alkhamis jioni kwamba tulikuwa tayari kuanzisha mazungumzo mapya bungeni kujadiliana kitu cha kufanya, lakini hakutaka mazungumzo yoyote kuhusu mpango mpya. Unajuwa kwa sababu gani, kwa kuwa aliona hilo ni jambo baya na badala yake akatumia mwanya huo, kuchukuwa likizo yake." Alisema.

Uamuzi wa vyama vya Forza Italia na League kujizuwia kupiga kura siku ya Alkhamis ulilenga kujibu uamuzi kama huo uliochukuliwa na mshirika kwenye serikali ya mseto - Vuguvugu la Nyota Tano, M5S.

Uamuzi wa M5S ulimfanya pia Draghi kuwasilisha barua ya kujiuzulu na hivyo hatua yake ya jana kujiuzulu ilikuwa ya pili ndani ya wiki moja. 

Uchaguzi mpya 

Italien I Der italienische Ministerpräsident Mario Draghi im Parlament
Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi amelazimika kujiuzulu kwa mara ya pili ndani ya wiki moja.Picha: Andrew Medichini/AP/picture alliance

Vyama vinavyounda serikali ya mseto ya Italia vilikataa kumuunga mkono Draghi kwa madai kuwa mkuu huyo wa zamani wa Benki Kuu ya Ulaya amekuwa mkosoaji mkubwa wa Urusi ambayo kwa miezi mitano sasa imekuwa ikiendesha operesheni ya kijeshi ndani ya ardhi iliyoivamia ya Ukraine. 

Awali Draghi alikuwa amesema yuko tayari kuendelea kusalia kuwa waziri mkuu, lakini kwa sharti la kupata uungaji mkono wa vyama vyote vinavyounda serikali ya mseto.

Kwenye mahojiano yake na waandishi wa habari, Berlusconi alisema chama chake hakijapiga kura ya kumkataa Draghi, bali kimezuwia tu kupiga kura. 

Sasa uchaguzi mpya umepangwa kufanyika tarehe 25 Septemba, jambo linaloiingiza Italia kwenye mzozo mwengine wa kisiasa kukiwa na wasiwasi kwamba vyama vya kihafidhina na vinavyopinga Umoja wa Ulaya vinaweza kufanya tena vyema mara hii.