Ruto auondoa kabisa muswada wa fedha 2024
26 Juni 2024Akilihutubia taifa kwa mara ya pili tangu maandamano kulitikisa taifa kwa saa kadhaa zilizopita, rais William Ruto alisisitiza kuwa amesikiliza kilio cha wakenya na kwamba wao ndio muhimu.
Rais Ruto pia ametangaza hatua za kubana matumizi ili kuweza kumudu mahitaji ya serikali na taifa kwa jumla. Ruto aliyebadili kauli na kuwa mpole, alitoa pia rambirambi kwa jamaa za waandamanaji waliopoteza maisha kwenye purukushani za hapo jana. Kiongozi wa taifa alisisitiza kuwa bado azma ya kufanya majadiliano na vijana iko palepale kwani anajali maslahi yao. Kauli hizo zinaungwa mkono na Askofu Dr Charles Marita ambaye ni mwenyekiti wa baraza la maaskofu tawi la Nakuru.
Waandamanaji wavamia jengo la bunge Kenya
Ifahamike kuwa bunge la taifa lilianza likizo hii leo hadi wiki ya mwisho ya mwezi ujao wa Julai. Yote hayo yakiendelea, vikosi vya jeshi la taifa vinaendelea kupiga doria kwenye ikulu na sehemu muhimu za serikali katika miji mikuu ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nakuru. Tayari chama cha mawakili nchini Kenya, LSK kimeanzisha mahakamani mchakato wa kushinikiza jeshi hilo kuondoka mitaani. Mchakato ambao utaanza rasmi kesho Alhamisi. Jeshi limekuwalikipiga doria tangu usiku wa kuamkia leo.
Ada ya matibabu ya waliojeruhiwa yafutiliwa mbali
Kwa upande mwengine, kaunti ya Nairobi imefutilia mbali ada za matibabu kwa waliojeruhiwa kwenye vurugu za maandamano na pia za kuhifadhia maiti kwenye chumba cha serikali cha City.
Kwa mujibu wa waziri wa afya wa kaunti ya Nairobi, Suzanne Silantoi,agizo hilo ni la gavana Johnson Sakaja na kwamba kufikia sasa watu wasiopungua 12 walipoteza maisha yao jana.Maiti hizo zilifikishwa kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti vya City na hospitali ya Mama Lucy. Watetezi wa haki za binadamu wamekosoa matumizi ya nguvu yaliyochangia maafa maandamanoni.
Kenya yafanya tathimini ya hali baada ya Maandamano
Hatimaye, mahakama ya Eldoret imesitisha operesheni zake kwa muda baada ya hati muhimu kuharibiwa kwenye maandamano ya Jumanne.Mahakama hiyo iko pembeni ya maktaba ya taifa mjini humo iliyotiwa moto na waandamanaji.
Thelma Mwadzaya, DW Nairobi