1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto alia na mabadiliko ya tabianchi, ataka kodi ya kaboni

5 Septemba 2023

Rais wa Kenya William Ruto amesema Mabadiliko ya Tabianchi yanatafuna maendeleo ya kiuchumi ya Afrika na ni wakati wa kuwa na mazungumzo ya kimataifa kuhusu kodi itakayotozwa wachafuzi wa mazingira.

https://p.dw.com/p/4Vz6r
Kenya Nairobi | Mkutano wa Kilele wa Mazingira Afrika | William Ruto, Rais wa Kenya
Rais wa Kenya William Ruto ataka wachafuzi wakubwa wa mazingira walipie.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Kwa mujibu wa rais Ruto, bara linalokua kwa kasi la Afrika lenye wakazi bilioni 1.3 linapoteza asilimia 5 hadi 15 ya ukuaji wa pato lake jumla la ndani kila mwaka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, akiutaja upotevu huu kuwa chanzo cha mfadhaiko mkubwa katika bara hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali na ambalo linachangia kidogo sana kwenye ongezeko la joto la dunia.

Hotuba za ufunguzi wa mkutano huo zimejumuisha wito wa wazi wa kufanya mageuzi ya mifumo ya fedha duniani ambayo imeaacha mataifa ya Afrika yakilipa takriban mara tano zaidi ya kwenye pesa za mkopo kuliko mengine, na hivyo kuzidisha mzozo wa madeni kwa wengi. Waziri wa Mazingira wa Kenya Soipan Tuya, amesema Afrika ina zaidi ya nchi 30 zenye madeni zaidi duniani.

Soma pia: Guterres aitaka dunia kuifanya Afrika kuwa nguvu ya nishati jadidifu

Mjumbe wa serikali ya Marekani kuhusu tabianchi, John Kerry, amekiri juu ya deni kubwa na lisilo la haki, na kuongeza pia kwamba mataifa 17 kati ya 20 duniani yalioathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi yako barani Afrika,  wakati mataifa 20 tajiri zaidi duniani, likiwemo lake, yanazalisha asilimia 80 ya hewa ukaa duniani ambayo inasababisha mabadiliko ya hali ya hewa.

Alipoulizwa kuhusu mwito wa rais wa Kenya wa mjadala wa ushuru wa kaboni, Kerry alijibu kwamba Rais Joe Biden "bado hajaidhinisha utaratibu wowote maalum wa kuweka bei ya kaboni."

Nairobi, Kenya | Mkutano wa Tabianchi wa Afrika 2023 | William Ruto, Rais wa Kenya
Rais William Ruto amezishauri nchi za Afrika kukumbatia uchumi rafiki kwa mazingira kabla ya kukuza viwandaPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Uchumi wa Kijani Afrika

Ruto alisema nchi 54 za Afrika "lazima zikumbatia haraka teknolojia rafiki kwa mazingira kabla ya kukuza viwanda na si kinyume chake, tofauti na anasa yaliokuwa nayo mataifa tajiri kufanya hivyo."

Kubadilisha uchumi wa Afrika katika mwelekeo wa kijani "ndio njia inayowezekana zaidi, ya haki na yenye ufanisi ya kufikia ulimwengu wa kiwango sifuri cha gesi ya ukaa ifikapo mwaka 2050," alisema.

Ufadhili wa tabianchi ni muhimu, wasemaji walisema, huku ahadi ya mataifa tajiri ya dola bilioni 100 kwa mwaka katika ufadhili wa hali ya hewa kwa nchi zinazoendelea ikiwa bado haijatekelezwa. Ruto alisema tamko la mkutano huo "litahimiza" kila mtu kutimiza ahadi zao.

Soma pia: Bomba la mafuta la Afrika Mashariki lakabiliwa na mtikisiko

Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao utakuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi, ulitangaza kuwa unapanga kuwekeza dola bilioni 4.5 katika "nishati safi" ya Afrika.

Uwezo wa nishati jadidifu wa Afrika

Bara la Afrika lina asilimia 60 ya rasilimali za nishati jadidifu duniani, na zaidi ya asilimia 30 ya madini muhimu kwa teknolojia inayoweza kurejelewa na zenye kaboni kidogo. Lengo moja la mkutano huo ni kubadilisha simulizi kuhusu bara la Afrika kutoka mwathirika hadi mshirika mwenye msimamo, tajiri.

"Inazidi kuwa vigumu kuwaeleza watu wetu, hasa kwa vijana wetu, kuhusu mkanganyiko: bara lenye rasilimali nyingi na watu maskini," Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde alisema.

Kenya Nairobi | Mkutano wa Tabianchi wa Afrika 2023 | John Kerry, Mjumbe wa Marekani
Mkutano wa Kilele wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Afrika ndiyo wa kwanza kabisaa kuandaliwa barani humo.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Pato la jumla la Afŕika linapaswa kuthaminiwa upya kutokana na mali zake zinazojumlisha msitu wa pili kwa ukubwa duniani wa mvua na bio-anuwai, alisema rais wa Benki ya Maendeleo ya Afŕika, Akinwumi Adesina. "Afrika haiwezi kuwa tajiri wa asili na maskini wa fedha," alisema.

Mabishano kuhusu nishati ya mafuta

Lakini mgawanyiko ni dhahiri kuhusu suala ambalo liligusiwa kidogo tu katika hotuba za ufunguzi na bado ni kiini cha mazungumzo magumu mbeleni: nishati ya mafuta.

Soma pia: Viongozi wa Afrika wakutana kujadili masuala ya mazingira

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika alisema Afrika lazima itumie rasilimali zake za gesi asilia - suala la maslahi yanayoongezeka ya Ulaya - pamoja na vyanzo vya nishati jadidifu. "Tupeni nafasi ya kukua," alisema.

Ruto, hata hivyo, amekosoa "uraibu" wa nishati ya mafuta. Nchi yake sasa inapata zaidi ya asilimia 90 ya nishati yake kutokana na nishati mbadala.

"Sio lazima tufanye kile ambacho nchi zilizoendelea zilifanya ili kuimarisha viwanda vyao. Itakuwa vigumu zaidi kutumia nishati jadidifu pekee, lakini inaweza kufanyika," alisema mshiriki mmoja wa ndani wa mkutano huo, Martha Lusweti.

Wakati wa kuvuja uraibu wa mafuta

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliuambia mkutano huo kuwa ni wakati wa "kuvunja uraibu wetu wa nishati ya mafuta." Ulimwengu ulitumia dola trilioni 7 kwa ruzuku ya mafuta mnamo 2022, kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen alisema mataifa ya Afrika yanaweza kuzalisha nishati safi ya kutosha kuliwezesha bara hilo na kusafirisha nje ya nchi, "lakini kwa hili, Afrika inahitaji uwekezaji mkubwa."

Baadhi ya mataifa makubwa kiuchumi barani Afrika yanategemea nishati ya mafuta. Viwanda vya Afrika Kusini vinavyotumia makaa ya mawe vinakumbwa na changamoto lukuki.

Sehemu za Delta ya Mto Niger zimeathirika kutokana na uchimbaji wa mafuta. Baadhi ya miji ya Afrika ina uchafuzi mbaya zaidi wa hewa duniani. Mradi wa bomba la TotalEnergies nchini Uganda na Tanzania unakabiliwa na changamoto.

Waliokosekana kwenye mkutano huo ni viongozi wa mataifa kadhaa yenye uchumi mkubwa barani Afrika ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, Nigeria na Misri, pamoja na Kongo yenye utajiri wa misitu.

Pia China ni miongoni mwa wazungumzaji wakuu wanaokosekana, ikiwa ni nchi inayotoa gesi nyingi zaidi zinazozuia joto duniani, mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara barani Afrika na mmoja wa wadai wake wakubwa.

Kerry ataka ushirikiano zaidi na China

Mjumbe wa Tabianchi wa Marekani John Kerry amesema anatumai Washington na Beijing "zinaweza kuja pamoja" katika vita dhidi ya ongezeko la joto duniani, katika mkutano huo unaolenga kukuza uwezo wa Afrika kama bara lenye nguvu ya kijani.

Matamshi ya Kerry yamekuja baada ya mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati kuzitaka Marekani na China kuweka kando tofauti zao na kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa, akionya kwamba migogoro ya kijiografia inaweza kurudisha nyuma mabadiliko ya nishati safi.

Kenya Nairobi | Mkutano wa Tabianchi wa Afrika 2023 | John Kerry, mjumbe wa Marekani
Mjumbe Maalumu wa Tabianchi wa serikali ya Marekani, John Kerry, amekiri juu ya ukosefu wa usawa katika mkutano wa ACS23 mjini Nairobi.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Mkuu huyo Fatih Birol alisema katika mahojiano na shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu kwamba mvutano wa kisiasa wa kijiografia ulikuwa kizuwizi kikubwa kwa sababu ushirikiano wa kimataifa kati ya wadau wakuu utakuwa changamoto zaidi.

Alizitaka China na Marekani kuweka kando mivutano yao ya kisiasa ya kijiografia na kiuchumi ili kutafuta misimamo ya pamoja au angalau inayofanana kuhusu masuala muhimu katika mkutano wa mazingira wa COP28unaofanyika baadae mwaka huu katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mkutano huo wa siku tatu wa kilele wa Nairobi, uliofunguliwa Jumatatu, umehudhuriwa na wakuu wa nchi, serikali na viwanda kutoka barani Afrika, pamoja na mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.

Chanzo: Mashirika