Bomba la mafuta la Afrika Mashariki lakabiliwa na mtikisiko
13 Aprili 2022Shinikizo lisilopungua kutoka makundi ya kutetea mazingira, chini ya Hashtag ya #StopEACOP, limepelekea benki zaidi na kampuni za bima kujiondoa kwenye ufadhili wa mradi wa bomba hilo la mafuta.
Wiki hii tu mradi huo ulipata pigo kubwa baada ya kampuni ya bima Allianz Group kujiondoa, ikiungana na benki 15 na makampuni saba ya bima, ambayo ni pamoja na HSBC, BNP Paribas na Swiss Re, ambayo yamekataa kutoa ufadhili wa kifedha kwa mradi huo kufuatia kampeni inayoendeshwa na mashirika kadhaa ya kutetea mazingira, yanayoongozwa na kundi la kimataifa la 350.org.
Soma pia: Samia, Museveni watia dole ujenzi wa bomba la mafuta
Bomba hilo la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443, linatajwa kuwa refu zaidi duniani lenye joto. Shirika la Taifa la Mafuta la China na kampuni ya nishati ya Ufaransa ya TotalEnergies, sambamba na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda na Kampuni ya Maendeleo ya Petroli Tanzania, zimeendelea kusimama kidete katika kuendeleza mradi wa bomba hilo linalotarajiwa kuanza kusafirisha mafuta mwaka 2025.
Johnson Nderi mchambuzi wa masuala ya kifedha mjini Nairobi anaunga mkono bomba la mafuta, akisema Afrika inahitaji umeme wa uhakika na wa bei nafuu kama unaotokana na mafuta na makaa ya mawe, ili kukuza sekta yake ya utengenezaji.
TotalEnergies yajitetea
Shirika la 350.org linadai kuwa ujenzi wa bomba hilo utahamisha maelfu ya familia na kutishia rasilimali za maji katika mabonde ya Ziwa Victoria na Mto Nile. Shirika hilo la mazingira linasema bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi litazalisha takribani tani milioni 37 za hewa ukaa kila mwaka, na hivyo kuchochea mabadiliko ya tabianchi.
Soma pia:Uganda na Tanzania zasaini mkataba ujenzi wa bomba la mafuta
Omar Elmawi, mratibu wa kampeni ya #StopEACOP, ameishutumu kampuni ya mafuta ya TotalEnergies, kuwa kuweka faida juu ya watu, akisema jamii nchini Uganda na Tanzania zimekuwa zikipambana bila kuchoka dhidi ya bomba hilo, na tayari mkururo wa uharibifu unadhihirika wazi.
Elmawi amesema wakati ambapo wanasayansi wanatoa wito wa kusitishwa kwa miradi ya mafuta, ili kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi, haishauriwi na ni kutowajibika kuendelea na mradi huo, huku wakipuuza vilio vya wale walioathirika zaidi.
Kampuni ya TotalEnergies imetetea bomba hilo ikibainisha kuwa inazingatia kikamilifu sheria za mazingira za Uganda na Tanzania. Ripoti ya tathmini ya athari za kijamii kwa mazingira iliyofanywa na tume ya Uholanzi ya tathmini ya mazingira iliibua wasiwasi kuhusu hatari kubwa kwa wanyamapori hasa sokwe katika hifadhi za misitu za Bugoma, Wambabya na Taala.
Soma pia: Matamshi ya Rais Magufuli yazusha hisia mseto Uganda
Bomba hilo la chini ya ardhi ambalo awali lilikadiriwa kugharimu dola bilioni 3.5, hivi sasa litagharimu dola bilioni 5 na linatrajiwa kuanzia karibu na Ziwa Albert katika wilaya ya Hoima, magharibi mwa Uganda. Litazunguka Ziwa Victoria na kuingia kaskazini mwa Tanzania likielekea rasi ya Chongoleani iliyoko bahari ya Hindi, likisafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku.
Chanzo: APE