1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripota wa Aljazeera auawa Ukingo wa Magharibi

11 Mei 2022

Ripota wa kituo cha televisheni cha kimataifa cha Aljazeera amepigwa risasi na kuuawa wakati wa uvamizi wa Israel katika eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi leo. Kituo hicho kimeishutumu Israel kwa kumuua.

https://p.dw.com/p/4B7we
Palästina | Journalistin Shireen Abu Akleh durch Schüsse getötet
Picha: Al Jazeera Media Network/AP/picture alliance

Aljazeera imesema ripota wake Shireen Abu Aqleh, raia wa Marekani mwenye asili ya Palestina aliekuwa na umri wa miaka 51, alikuwa amevaa kizibao cha waandishi habari kilichomuonyesha wazi kuwa mwandishi habari wakati akiripoti katika mji wa Jenin.

Alikuwa akiripoti juu ya uvamizi unaoendelea wa vikosi vya Israel katika Ukingo wa Magharibi, ulioanzishwa katikati mwa mashambulizi makali ya mitaani ya watu wa jamii ya Kiarabu nchini Israel.

Soma zaidi: Israel yaanzisha msako kufuatia mauaji katika mji wa Orthodox

Aljazeera imesema ripota huyo alilengwa maksudi, huku ofisi ya waziri mkuu wa Israel Nafatli Bennett ikisema katika taarifa kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa Abu Aqleh aliuawa kwa risasi zilizofyatuliwa na Wapalestina.

Palästina | Journalistin Shireen Abu Akleh durch Schüsse getötet
Shireen Abu Aqleh enzi za uhai wake.Picha: Al Jazeera Media Network/AP/picture alliance

"Kuna viashiria kwamba bibi Abu Aqleh aliuawa kwa risasi za magaidi wa Palestina. Israel itaendelea kufanya uchunguzi wa kina. Tunatoa wito kwa Mamlaka ya Palestina kutoa ushirikiano kwa uchunguzi huo ili kupata ukweli," alisema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Israel, Lior Haiat.

Hata hivyo Mamlaka ya Palestina, ambayo inasimamia baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibina inashirikiana na Israel kwenye masuala ya usalama, imetupilia mbali pendekezo hilo na kulaani kile ilichokiita uhalifu wa kutisha uliofanywa na vikosi vya Israel.

Soma pia: Jeshi la Israel lashutumiwa kumuua kijana wa kipalestina

Wizara ya Afya katika Ukingo wa Magharibi imesema Abu Aqleh alipigwa risasi kichwani, na alitangazwa kufariki dunia mara baada ya kufikishwa hospitalini.

'Wametulenga kwa maksudi'

Palästina | Journalistin durch Schüsse getötet
Waombolezaji na wanaume wenye silaha waliofunika nyuso zao wakibeba jeneza la mwandishi wa Aljazeera Shireen Abu Aqleh, alieuaw ana wanajeshi wa Israel akiwa kazini katika Ukingo wa Magharibi, Mei 11, 2022.Picha: Jaafar Ashtiyeh/AFP/Getty Images

Mfanyakazi mwingine wa Aljazeera, Ali Samoudi, ambaye pia alipigwa risasi mgongoni, lakini akiripotiwa kuwa katika hali nzuri, amesema alikuwa na Abu Akleh na waandishi wengine katika shule za kambi ya wakimbizi ya Jenin, wote wakiwa wamevalia vizibao vya wana habari wakati walipolengwa na wanajeshi wa Israel.

Amesema wanajeshi hao walijua fika kwamba wote waliokuwepo eneo hilo walikuwa waandishi na kwamba hakukuwa na watu waliojihami kwa silaha katika eneo hilo au hata makabaliano yoyote ya silaha, na kusisitiza kuwa wamelengwa kwa maksudi.

Soma pia: Jeshi la Israel ladaiwa kutekeleza mauaji Ukingo wa Magharibi

Salaam za rambirambi zimetolewa kutoka kote katika ulimwengu wa Kiarabu, ambako mwandishi huyo wa siku nyingi alikuwa mashuhuri kutokana na kuripoti juu ya Wapalestina.

Balozi wa Marekani nchini Israel, Tom Nides, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba amehuzunishwa sana na kifo cha Abu Aqleh na kutoa wito wa uchunguzi wa kina, huku akithibitisha kwamba ripota huyo alikuwa raia wa Marekani.

Chanzo: Mashirika