Israel yaanzisha msako baada ya mauaji mjini Elad
6 Mei 2022Shambulio la Alhamisi usiku huko Elad, mji wa katikati mwa Israel ulio na idadi kubwa ya Wayahudi wa madhehebu ya Orthodox, lilikuwa la sita katika mashambulizi ambayo Waisraeli wanalengwa tangu Machi 22 mwaka huu.
Mashuhuda wa tukio hilo wameliambia shirika la habari la AFP kwamba washambuliaji wawili waliokuwa wakining´inia kwenye gari, waliwashambulia kwa shoka wapita njia na kusababisha vifo vya watu watatu huku wanne wakijeruhiwa, kabla ya kukimbia kwa kutumia gari hilo.
Soma pia: Makabiliano mapya yazuka kwenye msikiti wa al-Aqsa
Shambulio hilo limekuja saa chache baada ya mapigano kati ya Waisraeli na Wapalestina katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa, eneo ambalo linazozaniwa mno katika mji wa Kale wa Jerusalem unaokaliwa kwa mabavu na Israel na ambalo limekuwa kivotu cha ghasia kwa majuma kadhaa.
Wapalestina wamekasirishwa na kuongezeka kwa ziara za Wayahudi kwenye uwanja wa Al-Aqsa, ambapo kwa makubaliano ya muda mrefu, Wayahudi wanaweza kutembelea eneo hilo lakini hawaruhusiwi kufanya ibada. Israel imesema makubaliano hayo hayatabadilika.
Tukio hilo lalaaniwa kimataifa
Shambulio la Elad limelaaniwa na Marekani pamoja na rais wa Palestina Mahmud Abbas, ambaye alionya kuwa huenda likasababisha kuongezeka kwa ghasia.
Lakini Hamas na kundi jengine lenye silaha la Palestina la Islamic Jihad, walisifu shambulio hilo, na kulitaja kuwa ni matokeo ya machafuko ya Al-Aqsa. Hata hivyo hakuna kundi lolote hadi sasa ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo.
Vikosi vya usalama vya Israel vimeanzisha msako mkali wa kuwatafuta washambuliaji, waliotambuliwa na polisi kama Assad Yussef al-Rifai na Subhi Imad Abu Shukair, wakiwa na umri wa miaka 19 na 20.
Soma pia:Wakristo waanza maadhimisho ya Pasaka
Wakati helikopta na ndege zisizo na rubani zikiunguruma kuwatafuta wahalifu hao, vijana wa Kiyahudi waliovalia mashati meupe wameonekana wakijumuika pamoja na kuimba karibu na eneo kulikotokea shambulizi hilo.
Polisi wamewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu washukiwa hao baada ya kuchapisha picha na majina yao. Wanatajwa kuwa ni wakaazi wa kijiji cha Rummanah karibu na mji wa Jenin eneo la Ukingo wa Magharibi.
'Magaidi' kukamatwa na kuwajibishwa
Waziri wa Ulinzi wa Israel Benny Gantz alitangaza hatua za kuwazuia washukiwa hao kutoroka. Nae Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett amesema magaidi watakamatwa na kuhakikisha wanalipa gharama.
Waliofariki wametambuliwa na vyombo vya habari vya Israeli kuwa ni Yonatan Habakuk, (44) na Boaz Gol,(49), kutoka Elad, pamoja na Oren Ben Yiftah, mwenye umri wa miaka 35 kutoka katikati mwa jiji la Lod.
Soma pia: Al-Aqsa: Waislamu watilia shaka hatua za Israel
Kabla ya tukio hilo la Alhamisi, mfululizo wa mashambulizi tangu Machi 22 ulisababisha vifo vya watu 15 katika maeneo tofauti ndani ya Israel.
Jumla ya Wapalestina 27 na Waarabu watatu waIsrael wamekufa katika kipindi hicho, miongoni mwao wakiwemo wahusika wa mashambulizi na wale waliouawa na vikosi vya usalama vya Israel katika operesheni za Ukingo wa Magharibi.
Kwa Wapalestina, kumbukumbu ya mwaka wa 1948 ya tangazo la uhuru wa Israeli ni alama ya "Nakba" au janga, wakati zaidi ya Wapelestina 700,000 walikimbia au kufukuzwa wakati wa vita vilivyotokana na kuundwa kwa Israel.
(AFPE)