1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia zaendelea

Admin.WagnerD15 Septemba 2015

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameutaka Umoja wa Mataifa uingilie kati ili kuutatua mgogoro uliozuka kwenye eneo la msikiti wa Al-aqsa katika mji wa Jerusalem

https://p.dw.com/p/1GWtG
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas
Rais wa Palestina Mahmoud AbbasPicha: Reuters/B. Ratner

Leo ni siku ya tatu tangu mapambano yaanze baina ya polisi na Waislamu kwenye eneo la msikiti wa Al-Aqsa

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Rais, Bwana Erdogan amemwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki-moon kwa njia ya simu kwamba polisi wa Israel wamelivamia eneo la msikiti wa al-Aqsa, kitendo ambacho hakiwezi kukubalika. Rais Erdogan amesema hatua ya polisi wa Israel inasababisha ghadhabu miongoni mwa Waislamu.

Na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amefahamisha kwamba,Ban Ki-moon ameingiwa wasi wasi juu ya kuongezeka kwa ghasia kwenye eneo la msikiti wa al_Aqsa . Msemaji huyo ameeleza kwamba yanayotukia kwenye msikiti wa al-Aqsa, kwa mara nyingine yanaonyesha ulazima wa kufikia makubaliano kwa njia ya mazungumzo juu ya masuala yote, ikiwa pamoja na kuweka taratibu zitakazokubalika kwa wote juu ya sehemu hiyo takatifu.

Radio ya Israel imeripoti kwamba Polisi wa Israel walilivamia eneo la msikiti na kuwakamata Wapalestina wawili. Polisi wamedai kwamba Wapalestina hao walikuwa wanarusha mawe na kwamba polisi watano walijeruhiwa kidogo .

Shirika la misaada la Wapalestina Hilali nyekundu limesema madaktari wake waliwatibu Wapalestina kadhaa waliojeruhiwa katika mapambano na Polisi.

Msemaji wa Polisi ya Israel ameeleza kwamba polisi waliingia kwenye eneo la msikiti mapema leo ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwamo ndani ya msikiti tokea jana usiku Kwa mujibu wa polisi waandamanaji walirusha mawe na fataki lakini polisi waliweza kuifungua sehemu hiyo na kuwawezesha Wayahudi kuingia.

Eneo takatifu kwa wote

Waislamu wanaliabudu eneo la msikiti wa al-Aqsa na wanaamini Mtume wa dini yao Muhammad alipaa mbinguni kutokea sehemu hiyo.Lakini sehemu hiyo pia inazingatiwa kuwa takatifu na wayahudi.

Mfalme wa Jordan Abdullah alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba kuzidi kwa uchokozi wowote kwenye eneo la msikiti wa al-Aqsa kutaathiri uhusiano baina ya Israel na Jordan.

Palästinenserpräsident Mahmud Abbas
Picha: Reuters

Msemaji wa Rais wa Palestina,Mahmoud Abbas ameonya kwamba hatua za Israel katika mji wa Jerusalem zinaweza kusababisha madhara makubwa.

Umoja wa Ulaya pia umetahadharisha juu ya kuongezeka mvutano baina ya polisi wa Israel na Wapalestina.

Marekani pia imeelezea wasi wasi juu ya matukio ya mjini Jerusalem.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani John Kirby amezitaka pande zote zijizuie kufanya vitendo vya uchokozi.

Mwandishi:Mtullya Abdu/afpe,rtre

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman