1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yapunguza vikwazo kwa Palestina mwezi wa Ramadhan

19 Juni 2015

Israel imetangaza kuwaondolea vikwazo kadhaa wapalestina wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, kama ishara ya nia njema wakati wa mwezi wa Ramadhan, ikiwamo fursa ya kuswali sala ya Ijumaa katika msikiti wa Al-Aqsa.

https://p.dw.com/p/1FjdW
Tempelberg Jerusalem Archiv Juni 2014
Picha: AFP/Getty Images/Ahmad Gharabli

Israel imetangaza siku ya Jumanne kuwa kwa mara ya kwanza itaondoa vikwazo vya usafiri ilivyowawekea Wapalestina na kuwaachia kusafiri baina ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi na ukanda wa Gaza, kama fursa maalumu kwa heshima ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Halikadhalika Baraza la Ulinzi la Israel Cogat linalohusika na masuala ya Palestina, limesema wiki hii kwamba litawaruhusu wakaazi wa Ukingo wa Magharibi na baadhi wa wakaazi wa ukanda wa Gaza kuhudhuria sala ya Ijumaa leo katika msikiti mtukufu wa Al-Aqsa ulioko mjini Jerusalem.

Kwa upande wa ukanda wa Gaza, kiasi cha wapalestina 800 wataruhusiwa kuhudhuria sala hiyo na kwa upande wa Ukingo wa Magharibi hakujatolewa idadi maalumu ila kwa wanaume ni wale wa miaka 40 na kupindukia na wanawake wa marika yoyote. Hii ikiwa ni Ijumaa ya mwanzo kwa waislamu wa Palestina walioanza mfungo wa mwezi wa Ramadhan jana Alhamisi.

Baraza hilo la Israel limesema pia litaweka mabasi maalumu ya kuwasafirisha watu hao na kuwapeleka katika msikiti wa Al-Aqsa kwa salaa ya Ijumaa.

Pamoja na hayo, Israel pia itawaruhusu wakaazi 200 wa Gaza kuwatembelea jamaa zao wanaoishi Ukingo wa Magharibi, na wakaazi 500 wa ukingo wa Magharibi wataruhusiwa kuingia katika ukanda wa Gaza.

Pia wakaazi 500 wa miji ya Ukingo wa Magharibi, wataruhusiwa kusafiri kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Israel Ben Gurion. Israel halikadhalika imetoa ruhusa kwa familia 300 kutoka nchi za nje, kutembelea jamaa zao wanaoishi katika ukanda wa Gaza.

Msemaji mkuu wa baraza la ulinzi la Israel la Cogat ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa hatua za namna hii ni muhimu kutokana na ushirikiano wa usalama unaoendelea baina ya Israel na mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa magharibi. Lakini pia amesema ukiukwaji wowote utakaotokea, utachukuliwa hatua.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/afpe

Mhariri:Josephat Charo