1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani bila matumanini ya kuleta amani kati ya Israel na Palestina

23 Desemba 2014

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anaumaliza mwaka wa 2014 kama alivyouanza, akiwa katika hali ya kukata tamaa licha ya jitihada zake za kuleta amani kati ya Israel na Palestina.

https://p.dw.com/p/1E91a
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters/E. Vucci

Katika wiki chache zilizopita wakati harakati za kidiplomasia zikiwa zinaendelea kwa upande wa nchi za Kiarabu zikishinikiza Israel kutoka katika ardhi ya Wapalestina ndani ya miaka mitatu ijayo, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry aliwasili Jordan kwa matumaini ya kupata suluhisho mbadala ambayo ingeleta amani kwa pande zote mbili.

Kuanzia Januari ya mwaka huu, Kerry alikuwa katikati ya mazungumzo ya amani ambayo yalitarajiwa kumalizika mwishoni wa mwezi wa April. Waziri huyo aliuanza mwaka 2014 kwa safari ya Jerusalem ambapo alikabiliana na wandamanaji wa Kipalestina, ujenzi mpya wa makaazi ya Waisrael katika maeneo ya Wapalestina, pamoja na upinzani mkali kutoka kwa maafisa wa Kimarekani waliosema kuwa uongozi wa Obama unashindwa kuleta suluhisho kupitia njia ya mazungumzo.

Italien USA Israel Außenminister John Kerry trifft Benjamin Netanyahu in Rom
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Isreal Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/E. Vucci

Katika jitihada zake Kerry alijaribu kumshawishi Waziri Mkuu wa Isreal Benjamin Netanyahu kuonesha ishara ya nia njema kwa Wapalestina kwa kuwaachia huru wafungwa wa Kipalestina, lakini hilo halikutokea.

Vile vile, Kerry alijaribu kumshawishi Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kuitambua Isreal kama taifa la Kiyahudi, naye Abbas alilikataa hilo.

Hatimaye mzozo ulizidi kupamba moto pale Israel iliposonga mbele na mpango wa kujenga makazi katika eneo lilioko mashariki mwa Jerusalem, eneo ambalo Wapalestina wanadai kuwa ni lao.

Muda mfupi baadaye Abbas alikubaliana kuunda serikali ya umoja pamoja na mahasimu wake wa kisiasa Hamas, kikundi ambacho Israeli na Marekani wanakitambua kuwa cha kigaidi. Kwa hasira Israel ilijitoa katika mazungumzo ya amani.

Kerry und Abbas in Ramallah
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na Rais wa Palestina Mahmoud AbbasPicha: Reuters

Baada ya hapo mambo yalizidi kuwa mabaya, uongozi wa Obama ulionya kwamba kusitishwa kwa mazungumzo ya amani kunaweza kusababisha vuguvugu jipya la upinzani kwa upande wa Palestina.

Kufikia mwezi wa Juni machafuko yalizuka, ambayo yalijumuisha utekaji nyara na vifo vya vijana watatu wa Kiisrael vilivyodaiwa kuwa ni kazi ya Hamas. Kilichofatia ni mauaji ya kisasi ya kijana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 16 yaliyofanywa na Waisrael wenye msimamo mkali.

Kufikia tarehe 8 mwezi wa Julai kulizuka vita baina ya Waisrael na Wapalestina vilivyodumu kwa siku 50 katika ukanda wa Gaza. Vita hivyo viliua takriban Wapaestina 2,100 na Waisrael 72.

Vita vikiwa bado vinaendelea katika mwezi wa Agosti, Kerry aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kuwa makubaliano yamekwishafikiwa baina ya pande hizo mbili. Mapigano yalisita masaa mawili tu baadae, ingawa mvutano huo bado uliendelea na kufikia mwezi wa Novemba vurugu zilianza tena.

Vurugu hizo zilitokea baada ya Waisrael kuwazuia Waislamu wa Kipalestina kuingia katika eneo takatifu la Jerusalem ulipo msikiti wa al-Aqsa. Hili lilianzisha tena mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina.Kutokana na hayo, nchi jirani Jordan iliondoa ubalozi wake mjini Tel Aviv .

Jerusalem Felsendom
Mskiti wa al-Aqsa mjini JerusalemPicha: DW/T. Kraemer

Halikadhalika kitendo cha Jordan kuwakilisha ombi la viongozi wa Palestina kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalopendekeza kuwa Israel ihame kwenye maeneo yao ifikapo mwaka 2017, kitaharibu zaidi uhusiano baina ya Israel na Jordan.

Kulikuwa na matarajio makubwa juu ya Kerry, iliaminika kwamba angeweza kuleta mbinu mpya za kupatikana amani kati ya Isreal na Palestina. Sasa wadadisi wa Mashariki ya kati pamoja na Washington wanastaajabu kwa nini Kerry hata alijaribu kutaka kuleta amani, kwani kazi hiyo inaelekea kumshinda.

Mwandishi: Yusra Buwayhid /APE

Mhariri: Gakuba Daniel