Rais Ruto alegeza msimamo dhidi ya idara ya Mahakama
16 Januari 2024Rais William Ruto ameridhia kufanya mazungumzo na idara ya mahakama siku moja baada ya jaji mkuu wa mahakama Martha Koome kumtaka kufanya mashauriano ili kusitisha mashambulizi yanayoendelezwa dhidi ya mahakama. Jaji Koome alionya kuwa matamshi ya viongozi serikalini kuwa watapuuza hukumu za mahakama huenda yakaibua msukosuko.
"Mashambulizi na matamshi haya ni ya kutia hofu na ni ukiukaji wa hali ya juu wa katiba. Ni mashambulizi dhidi ya sheria na utulivu wa taifa na yanaweza kusababisha machafuko na vurugu,” alisema Jaji Koome.
Ruto adai Kenyatta alikuwa na bajeti ya kuihonga mahakama
Kiongozi wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini COTU, Francis Atwoli hii leo amefanya kikao na majaji wa mahakama za kazi nchini ambapo ameitetea idara ya mahakama kama kiungo kinachomlinda mwananchi asiyejiweza, ingawa amesisitiza kuwa juhudi za kupambana na ufisadi lazima zipewe kipaumbele.
"Hii ni mahakama inayowalinda wanyonge kwa hiyo tutakuwa kwenye mstari wa mbele kuilinda mahakama, lakini hii haimaanishi kwamba tunaunga mkono ufisadi. Tunamuunga mkono Rais kwa asilimia 100, kupambana na ufisadi kwenye idara ya mahakama na vitengo vingine vyote,” alisema Francis Atwoli.
Vilevile, kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga amemkosoa Rais Ruto kwa kuitishia mahakama akiitaja kama njama ya kuiteka idara hiyo muhimu ya usimamizi wa sheria. Amewataka viongozi kujitokeza na kuwalinda wananchi dhidi ya ubadhirifu wa serikali akisema serikali imefeli kuangazia mambo yanayowaminya wananchi, hasa gharama ya juu ya maisha.
Kulingana na Jaji Koome, majaji waliotuhumiwa kwa ufisadi au utovu wa maadili wamekabiliwa kisheria huku wafanyikazi 71 wa idara hiyo wakifutwa kazi.
Wakio Mbogho, DW, Nakuru.