Ruto adai Kenyatta alikuwa na bajeti ya kuihonga mahakama
10 Januari 2024Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi kwa Mradi wa Nyumba za Bei Nafuu wa Kapsuswa katika Kaunti ya Uasin Gishu, Rais Ruto aliwakemea wakosoaji wa mradi wake wa majaribio akisisitiza kwamba hataogopa wala kutetereka katika azma yake ya kukomesha ufisadi katika idara ya mahakama.
Hayo yanajiri juma moja baada ya nyumba za wakazi wa mtaa wa Pioneer kubomolewa katika eneo hilo kwa lengo la kujengwa kwa nyumba za bei nafuu. Wakazi hao walidai kuwa hawakupewa ilani.
Rais aliwahi kuwa mjumbe wa eneo hilo kwa miaka kumi. Rais alisema serikali yake haitatenga bajeti ya kuwahonga maafisa katika idara ya mahakama.
Soma pia: Kenyatta: Serikali msilaumu utawala uliopita chapeni kazi
"Watu fulani wanasema kwamba kwa sababu serikali iliyopita ilikuwa na bajeti ya kuwahonga mahakama, nifanye na mimi bajeti ya kuwahonga mahakama. Je, mnataka pesa yenu itumike kuwahonga mahakama? Hakuna bajeti itakayotengenezwa kumhonga yeyote mahakamani. Mahakama ni watumishi wa Wakenya."
Asisitiza majaji wanakula rushwa
Rais Ruto, ambaye alionekana kuwa na hasira, alikariri matamshi yake ya awali kwamba baadhi ya watu walikuwa wakishirikiana na majaji kuvuruga miradi ya Kenya Kwanza kama vile nyumba za bei nafuu.
Aliwahakikishia wakazi kwamba atapambana na ufisadi katika idara ya mahakama, akiongeza kwamba hakuna mtu atakayekuwa na ruhusa ya kuondoa ajenda iliyokusudiwa kwa Wakenya.
Serikali inapania kujenga nyumba 20000 katika mji wa Eldoret pekee huku vijana elfu 50 wakiajiriwa. Wakazi wasio na uwezo watahitajika kulipa kati ya shilingi 4000 na 30 za Kenya kila mwezi ili kumiliki.
Rais aliandamana na Naibu wake Rigathi Gachagua ambaye alimuunga mkono.
Soma pia:Kenya: Mrengo wa chama cha Jubilee unaompinga Kenyatta wajitenga na Azimio la Umoja
"Wewe ulipewa ridhaa na hawa wananchi. Wenye kujenga ni hawa wenye kujengewa nyumba ni hawa. Hawa ndio wenye kusema. Hawa ndio matajiri wako mheshimiwa rais," alisena Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye aliambatana na Ruto, na kuongeza kuwa "watu ya kortni hawakukuajiri.
Mashambulizi ya Rais Ruto dhidi ya mahakama yanafanana na kile alichoelezea mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, ambaye pia alikuwa akikosoa majaji kwa kutoa dhamana kubwa kwa washukiwa wa ufisadi na kupokea rushwa.
Mara tu baada ya kuchukua madaraka, Ruto aliwateua majaji 41 ambao Uhuru alikuwa amekataa kuwaidhinisha, akisisitiza azma yake ya uhuru wa Mahakama na kuahidi uhusiano bora kati ya Utendaji na mahakama ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti kutoka Shilingi bilioni 17 hadi Shilingi bilioni 22.
Chama cha mawakili kilitishia kufanya maandamano ya amani juma hili kupinga matamshi hayo ya Rais ila maandamano hayo hayajashuhudiwa.