Berlin na Ankara: Mahasimu kisiasa, marafiki kiuchumi
16 Novemba 2023Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anafanya ziara nchini Ujerumani siku ya Ijumaa. Vita kati ya Israel na Hamas pamoja na masuala ya uhamiaji na biashara ni miongoni mwa masuala yatakayozingatiwa kwenye mazungumzo kati ya Erdogan na watawala wa Ujerumani.
Ziara ya Erdogan inafanyika muda mfupi baada ya rais huyo wa Uturuki kutoa maoni yake yenye utata kuhusu Israel mapema mwezi hu, ambapo aliishutumu Israel kwa "ufashisti" na "uhalifu wa kivita" na kisha kulisifu kundi la Hamas. Matamko hayo ya rais Erdogan yalisababaisha Israel kuwaondoa wanadiplomasia wake kutoka Uturuki.
Soma pia: Kansela Scholz akutana na Rais Erdogan
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliyakemea madai ya Erdogan dhidi ya Israel na akatangaza kuwa atalizungumzia hilo katika mkutano wake na kiongozi huyo wa Uturuki.
Ripoti ya Tume ya Ulaya ya hivi karibuni kuhusu Uturuki pia imeeleza kuwa msimamo wa rais wa Uturuki hauendani kabisa na mtazamo wa nchi za Magharibi.
Lakini licha ya kuwepo mizozo mingi katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Uturuki umeendelea kuimarika. Kwa miaka mingi, Ujerumani imekuwa ikizingatiwa kuwa mshirika muhimu zaidi wa biashara wa Uturuki na mwekezaji muhimu wa kigeni katika nchi hiyo.
Ujerumani na Uturuki zinategemeana
Uturuki inaagiza zaidi mashine, magari, bidhaa za plastiki, ndege, kemikali na vifaa vya matibabu kutoka Ujerumani.
Rais wa Wakfu wa Maendeleo ya Kiuchumi (IKV) nchini Uturuki Ayhan Zeytinoglu, amesema uhusiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Uturuki umekita mizizi na kwamba Uturuki inafurahia uhusiano mzuri kati yake na Ujerumani.
Wawakilishi wa wafanyabiashara wa Uturuki wanamtaka Rais Erdogan wakati wa ziara ya mjini Berlin, ajumuishe uboreshaji wa kisasa kwenye umoja wa forodha kati ya Umoja wa Ulaya na Uturukimiongoni mwa masuala mengine muhimu. Wamesema vilevile Ujerumani inapaswa kutumia ushawishi wake hapa.
Zeytinoglu amesisitiza kuwa kiwango cha biashara kinaweza kukua maradufu na kufikia hadi euro bilioni 90 ikiwa umoja wa forodha utaboreshwa na kuwa wa kisasa. Amesema anatumai kuwa baadhi ya hatua zitachukuliwa wakati wa ziara hii ya rais Erdogan nchini Ujerumani.
Kulingana na takwimu za Chama cha Wafanyabiashara wa Kijerumani wa Nje ya Nchi (AHK) wanaoendesha biashra nchini Uturuki, ni kwamba makampuni ya Ujerumani yaliwekeza takriban euro bilioni 11.5 nchini humo kati ya mwaka 2002 na mwaka 2022. Zaidi ya asilimia sita ya uwekezaji wote wa kigeni nchini Uturuki unatoka Ujerumani.
Soma pia: Miaka 60 tangu Ujerumani iwaalike Waturuki nchini mwao
Zaidi ya kampuni 8,000 za Ujerumani zinazomilikiwa au zinazoshughulika kwa ushirikiano katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, zinafanya kazi nchini Uturuki hasa katika shughuli za viwanda, biashara za rejareja, biashara za ifaa na mauzo.
Siasa zinaharibu uchumi
Hata hivyo, matamshi ya uongozi wa Uturuki yanaendelea kudhoofisha imani ya wawekezaji nchini humo. Mnamo Juni 2023, Erdogan alimteua Mehmet Simsek kama waziri wa fedha, akitumai atafaulu kupunguza mfumuko wa bei huku nchi ikipata faida nje ya nchi.
Simsek, mtaalam wa uchumi anayetambulika kimataifa na mwakilishi wa mbinu huria ya masoko anajaribu kuifanya Uturuki iaminike tena lakini haonekani kufanikiwa kwa sababu sarafu ya Uturuki, Lira inashuka kwa kasi tangu uchaguzi wa bunge na rais wa mwezi Mei.
Kabla ya uchaguzi euro moja ilikua sawa na lira 21.50 lakini kwa sasa ni zaidi ya Lira 31 ili kupata euro moja.
Wakosoaji wanasema pana haja ya Ujerumani na Uturuki kuelekeza juhudi zao kukabiliana na masuala magumu na wakati huo huo kuboresha mbinu katika mashauriano yanayohusu kutatua mizozo.