1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Erdogan ashinda duru ya pili ya uchaguzi Uturuki

29 Mei 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito wa mshikamano wa kitaifa leo Jumatatu baada ya kushinda duru ya pili ya uchaguzi wa kihistoria na kuongeza muda wa utawala wake wa miongo miwili hadi mwaka 2028.

https://p.dw.com/p/4RvQE
Türkei Wahlen Erdogan wieder gewählt
Picha: Depo Photos/IMAGO

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 69, amefanikiwa kuruka kiunzi cha mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi nchini humo na pia kuhimili ushindani mkali kutoka kwa muungano imara wa upinzani kuwahi kukikabili chama chake cha Kiislamu.

Maelfu ya watu wamemiminika barabarani kwa shangwe na nderemo wakati kiongozi muhimu zaidi katika historia ya kisasa ya Uturuki alipowaongoza wafuasi wake kwa nyimbo za ushindi nje ya Ikulu ya rais mjini Ankara.

Matokeo yaliyokaribia kukamilika yameonyesha Erdogan amemshinda mpinzani wake Kemal Kilicdaroglu kwa zaidi ya asilimia nne ya kura zilizohesabiwa. Kwa mujibu wa Baraza Kuu la uchaguzi, Erdogan amejizolea asilimia 52.14 ya kura huku mpinzani wake akipata asilimia 47.86.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Joe Biden amempongeza Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kufuatia ushindi wake katika duru ya pili ya uchaguzi.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Biden ameandika kuwa anatarajia kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kama washirika wa muungano wa kijeshi wa NATO katika masuala muhimu kati ya Ankara na Washington na ushirika katika kukabiliana na changamoto za kimataifa.

Hata hivyo, rais huyo wa Marekani hakugusia juu ya msuguano wa hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken pia amempongeza Erdogan kupitia mtandao wake wa Twitter. Blinken hasa amesifu idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura na amesifu pia kile alichokiita "tamaduni ya muda mrefu ya kidemokrasia ya Uturuki."