Putin asema uvamizi wa Ukraine Kursk haujawa na athari
2 Septemba 2024Akizungumza na wanafunzi katika mji wa Kyzyl, Rais Putin amesema vikosi vya Ukraine havikufanikisha lengo lake la kuvizuia vikosi vya Urusi, kupigana huko mashariki mwa Ukraine.
"Ndio.. kwanza kabisa iliwatia wasiwasi watu wetu. Watu, na hasa katika jimbo la Kursk wanapitia wakati mgumu sana. Lakini lengo kuu walilojiwekea adui zetu la kuzuia mashambulizi huko Donbas hawakulifanikisha," alisema Putin.
"Lakini kwa sasa suala sio tu kusonga mbele kwa mita 200 au 300, hatujawahi kuwa na kasi kama hiyo Donbas. Vikosi vya Urusi viko tayari kudhibiti maeneo sio ya mita 200 au 300, ila ni ya kilomita za mraba," aliongeza rais huyo ya Urusi.
Soma pia: Zelensky: Wanajeshi wetu wanatimiza malengo yao huko Kursk
Amesisitiza kuwa baada ya kushindwa kwa uvamizi huo, kitakachofuata ni mazungumzo ya amani.
Kumekuwa na mashambulizi makali ya ardhini kati ya pande hizo, huku Ukraine ikizidi kuingia katika jimbo la Kursk na Urusi nao wakizidi kusonga mbele kwenye jimbo la Donbas, mashariki mwa Ukraine.