1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yazuwia maandamano ya upinzani Kinshasa

27 Desemba 2023

Polisi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa imewazuwia waandamanaji kukusanyika siku ya Jumatano, baada ya kuandamana dhidi ya uchaguzi wa hivi karibuni katika taifa hilo tete la Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/4acUX
DR Kongo Kinshasa 2023 | Maandamano ya upinzani | ghasia
Polisi ikikabiliana na wafuasi wa upinzani walioandamana mjini Kinshasa, Desemba 27, 2023.Picha: John Wessels/AFP/Getty Images

Wanasiasa wakuu wa upinzani katika nchi maskini lakini yenye utajiri wa madini nchini DRC waliitisha maandamano hayo baada ya kukataa kura ya wiki iliyopita, ambayo ilikumbwa na ucheleweshaji mkubwa na mtafaruku wa ukiritimba.

Waziri wa mambo ya ndani wa Kongo Peter Kazadi alisema Jumanne serikali ilipiga marufuku maandamano hayo kwa sababu "yanalenga kuharibu mchakato wa uchaguzi."

Upinzani hata hivyo ulikuwa umewataka wafuasi wake kukusanyika karibu na bunge la kitaifa mjini Kinshasa na kuandamana hadi makao makuu ya tume ya uchaguzi nchini humo.

Makumi ya polisi wa kutuliza ghasia waliwekwa katika eneo hilo Jumatano asubuhi, kulingana na waandishi wa habari wa AFP.

Waliwafyatulia vitoa machozi wafuasi wa mwanasiasa wa upinzani Martin Fayulu, waliokuwa wamekusanyika mbele ya makao makuu ya chama chake. Karibu na hapo, waandamanaji vijana walichoma matairi.

DR Kongo Kinshasa 2023 | Maandamano ya upinzani | ghasia
Vijana wakionyesha ghadhabu zao wakati wakitawanywa na polisi mjini Kinshasa, Desemba 27, 2023.Picha: John Wessels/AFP/Getty Images

Vurumai za uchaguzi wa Desemba 20

Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba upinzani lazima usubiri kuchapishwa kwa matokeo ya awali ya kura na kushughulikia malalamiko kuhusu mchakato wa uchaguzi kwenye Mahakama ya Katiba.

Soma pia:Upinzani kuandamana Kongo licha ya marufuku ya serikali 

Karibu wapiga kura milioni 44 walijiandikisha kupiga kura mnamo Desemba 20 katika chaguzi zilizofanyika wakati mmoja za rais, wabunge wa kitaifa na wa mikoa, na madiwani wa manispaa.

Lakini tume ya uchaguzi ilipambana kufikisha vifaa vya kupigia kura kwenye vituo vya kupigia kura kwa wakati katika nchi hiyo yenye ukubwa takribani sawa na Ulaya Magharibi -- na kuwaacha baadhi ya watu bila fursa ya kupiga kura.

Muda wa kupiga kura uliongezwa rasmi kwa siku ili kufidia matatizo hayo, na hata kudumu hadi Siku ya Krismasi katika baadhi ya maeneo ya mbali. Upinzani ulidai kulikuwa na "vurumai kubwa" na kulaani kasoro.

Askofu mkuu wa Kinshasa vile vile alielezea uchaguzi kama "vurugu kubwa za kupanga".

Vurugu zinazohusiana na uchaguzi ni jambo la kawaida nchini DRC, ambayo ina historia ndefu ya utawala wa kimabavu na mapinduzi ya vurugu ya serikali.

DR Kongo Kinshasa 2023 | Maandamano ya upinzani | ghasia
Polisi wakiwarushia mawe waandamanaji mjini Kinshasa, Desemba 27, 2023.Picha: John Wessels/AFP/Getty Images

Matokeo yaliyotolewa mpaka sasa na tume ya uchaguzi yanaonyesha Rais aliye madarakani Felix Tshisekedi anaongoza pakubwa, baada ya asilimia 79 ya kura milioni sita kuhesabiwa.

Soma pia:Kongo yaanza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi 

Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60, ambaye aliingia madarakani mwaka 2019 baada ya makabidhiano ya kwanza ya amani ya mamlaka nchini humo, anagombea muhula wa pili wa miaka mitano.

Moise Katumbi, mgombea mwingine na gavana wa zamani wa mkoa wa kusini-mashariki wa Katanga, amepata takriban asilimia 14 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.

Anafuatiwa na Fayulu, mtendaji wa zamani wa kampuni ya kimataifa ya mafuta, ambaye anasema yeye ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa 2018 uliomwingiza madarakani rais wa sasa, huku asilimia nne ya kura zikiwa zimehesabiwa.