1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pezeshkian ashinda uchaguzi wa rais Iran

Josephat Charo
6 Julai 2024

Masoud Pezeshkian, waziri wa zamani wa afya alimshinda mpatanishi wa zamani wa Iran katika mzozo wa nyuklia, Saeed Jalili katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais.

https://p.dw.com/p/4hy3b
Iran | Masoud Pezeshkian
Rais mpya wa Iran Masoud PezeshkianPicha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Masoud Pezeshkian, waziri wa zamani wa afya alimshinda mpatanishi wa zamani wa Iran katika mzozo wa nyuklia, Saeed Jalili. Duru ya pili ya uchaguzi wa rais inaripotiwa kushuhudia idadi kubwa zaidi ya wapiga kura kuliko ya kwanza.

Masoud Pezeshkian, mwanasiasa wa msimamo wa wastani ambaye ameahidi kuifungua Iran kwa ulimwengu, ameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais, maafisa walisema mapema Jumamosi. (06.07.2024)

Soma zaidi: Masoud Pezeshkian ashinda uchaguzi wa rais Iran

Baada ya matokeo kutangazwa, katika kauli zake za kwanza, Pezeshkian aliulezea uchaguzi huo kama mwanzo wa "ushirikiano" na watu wa Iran. 

"Njia ngumu mbele yetu haitakuwa laini pasi na ushirikiano wetu na uaminifu," Pezeshkian alisema katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X. "Nawanyoshea mkono wangu."

Mgombea wa msimamo mkali alikabiliwa na kushindwa

Pezeshkian, mwenye umri wa miaka 69, alipambana na Saeed Jalili, mwenye umri wa miaka 58, mwanasiasa mwenye msimamo mkali ambaye ni mpatanishi wa zamani wa Iran na nchi za Magharibi katika mzozo wa nyuklia wa Iran. Duru ya pili ya uchaguzi ilifanyika kumchagua mrithi wa hayati rais wa Iran Ebraim Raisi aliyekufa katika ajali ya helikopta mnamo mwezi Mei mwaka huu pamoja na waziri wa mambo ya nje na maafisa wengine wa Iran. 

Iran | Wahlen Saeed Jalili
Saeed Jalili, mwanasiasa mwenye msimamo mkali ambaye ni mpatanishi wa zamani wa Iran na nchi za Magharibi katika mzozo wa nyuklia wa IranPicha: Majid Asgaripour/WANA/REUTERS

Soma zaidi:Iran na Bahrain zaridhia mazungumzo ya kurejesha mahusiano 

Pezeshkian, daktari mtaalamu wa upasuaji, alikuwa waziri wa afya kuanzia mwaka 2001 hadi 2005. Kampeni yake ilijikita katika kujenga upya uaminifu kati ya serikali na watu wa Iran, kupambana na hali ya kukata tamaa kufuatia matatizo sugu ya kiuchumi na ukandamizaji wa kisiasa. 

Ametetea mahusiani yenye tija na nchi za Magharibi kufufua mkataba wa nyuklia, akilenga kuitoa Iran kutokana na hali ya kutengwa. 

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Mfalme wa Saudi Arabia na mwanamfalme, pamoja na waziri mkuu wa India Narendra Modi na rais wa China, Xi Jinping, walikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza wa dunia kumpongeza Pezeshkian kwa kuchaguliwa kama rais wa Iran.

Idadi ya wapiga kura ilikuwa kubwa kuliko duru ya kwanza

Kwa mujibu wa mamlaka, Pezeshkian alishinda uchaguzi wa Ijumaa na kura milioni 16.3, huku Jalili akijikingia kura milioni 13.5.

Ripoti za awali kutoka kwa mamlaka zinaashiria asilimia 50 ya wapiga kura walijitokeza, idadi iliyo kubwa zaidi kuliko ile iliyoshuhudiwa katika uchaguzi wa duru ya kwanza.

Masoud Pezeshkian na Saeid Jalili
Masoud Pezeshkian na Saeid JaliliPicha: IRIB

Kuna vituo kiasi 60,000 vya kupigia kura na zaidi ya wapiga kura milioni 61 wenye haki ya kupiga kura nchini Iran, kati ya idadi jumla ya wakazi milioni 85. 

Uchaguzi wa viwango vya chini

Huku kukiwa hakuna mgombea aliyetarajiwa kuleta mageuzi makubwa kwa sera za ndani au za kigeni za Iran, kwa kuwa mamlaka makubwa yako mikononi mwa kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei, rais wa Iran atakuwa na jukumu la kumteua mrithi wa kiongozi huyo mkuu wa nchi. 

Wachambuzi wanasema, hata hivyo, kwamba ushindi wa Jalili, ambaye mara kwa mara amekuwa akitoa kauli za ukali kwa nchi za Magharibi, ungeleta sera ya upinzani ya ndani na nje kwa upande wa Iran. 

Soma zaidi: Wairan waelekea vituoni kumchagua rais mpya kumrithi Raisi

Wanasema kuwa Pezeshkian, ambaye alishinda kura asilimia 10 zaidi kuliko Jalili katika duru ya kwanza, huenda akatetea sera ya kigeni isiyo na misimamo mikali, kuwa wazi zaidi katika kuyafufua mazungumzo na dola kubwa kuurejesha mkataba wa nyuklia na kuwa huru zaidi katika mtazamo wake kwa masuala ya jamii kama vile uvaaji wa lazima wa hijabu kwa wanawake. Iran inawakandamiza wanawake wanaokiuka sheria ya uvaaji wa hijabu. 

Masoud Pezeshkian
Mwanamageuzi Masoud Pezeshkian amechanguliwa kuwa rais mpya wa Iran katika duru ya pili ya uchaguziPicha: Rouzbeh Fouladi/ZUMA Press Wire/picture alliance

Pezeshkian aliendelea kushikilia kwamba wakati wote anamchukulia Khamenei kama mamlaka ya mwisho kuhusu masuala yote ya nchi. Wakati wa kampeni yake, Pezeshkian aliahidi hatatekeleza mageuzi yoyote makubwa ya mfumo wa utawala wa kidini wa madhehebu ya Shia wa Iran. 

Uwezekano wa wapiga kura kutojali

Duru ya pili ya uchaguzi, iliyoitishwa baada ya wagombea kushindwa kupata asilimia zaidi ya 50 ya kura zote zilizopigwa Juni 28 katika uchaguzi ulioshuhudia idadi ndogo ya asilimia 40 ya wapiga kura wakishiriki, inakuja huku kukiwa na misuguano ya kikanda kuhusiana na vita kati ya Israel na washirika wa Iran, kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza na kundi la Hezbollah nchini Lebanon.

Iran pia iko chini ya shinikizo linaloendelea kutoka nchi za Magharibi kuhusu mpango wake wa nyuklia, ambao nchi nyingi zinahofia huenda ukawa ni kisingizio cha utengenezaji wa silaha za nyuklia. 

Soma zaidi. Wagombea wa urais wa Iran wakabiliana katika mdahalo wa mwisho

Katika masuala ya ndani, Iran inakabiliana na uchumi uliozorota kufuatia kipindi kirefu cha usimamizi mbaya na rushwa serikalini na vikwazo ilivyowekewa mnamo 2018 baada ya Marekani kujiondoa kutoka kwenye mkataba wa kihistoria wa nyuklia wa mwaka 2015 na mataifa sita yenye nguvu duniani.

Iran I 2024
Masoud Pezeshkian na mpatanishi wa zamani wa Iran na nchi za Magharibi katika mzozo wa nyuklia wa Iran Saeed JaliliPicha: Iranian State Tv/ZUMAPRESS/picture alliance

Idadi ya wapiga kura wanaojitokeza kwenye chaguzi Iran imeshuka katika kipindi cha miaka minne iliyopita, huku wakosoaji wakisema hii inadhihirisha kuporomoka kwa uungwaji mkono wa utawala wa kiongozi wa kidini huku masaibu ya kiuchumi yakiongezeka na uhuru wa kisiasa na kijamii kwa kiwango kikubwa ukidhibitiwa.

Uchaguzi wa 2021 uliomleta madarakani Raisi ilishuhudia asilimia 48 ya wapiga kura wakishiriki na uchaguzi wa bunge mwezi Machi asilimia 41 tu.

(Reuters, AP, AFP)