1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Pande hasimu zakubaliana kusitisha mapigano kwa wiki 1 Sudan

22 Mei 2023

Mashambulizi ya angani, milio ya risasi na miripuko viliutikisa mji Mkuu wa Sudan Khartoum Jumapili, kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki moja kati ya majenerali hasimu.

https://p.dw.com/p/4Reoa
Sudan Unruhe Konflikt
Picha: AFP via Getty Images

Makubaliano ya hivi karibuni yananuiwa kuwezesha misaada ya kiutu kufikishwa kwa raia walioathiriwa na vita vinavyoendelea kati ya pande hizo mbili hasimu.

Katika taarifa ya pamoja, Marekani na Saudi Arabia wanaoongoza juhudi za upatanishi kati ya pande hizo mbili za kijeshi, zimesema makubaliano hayo yanapaswa kuanza kutekelezwa hii leo usiku na kwamba makubaliano ya sasa hivi ni tofauti.

soma zaidi:Makubaliano ya kusitisha vita yaleta matumaini mapya Sudan

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Pembe ya Afrika, IGAD wote wamekaribisha makubaliano yaliyofikiwa hapo jana baada ya takriban watu 1000 kupoteza maisha katika vita hivyo, na zaidi ya wengine milioni moja wakikimbilia nchi jirani kama Ethiopia, Sudan Kusini na Chad.

Mamilioni ya raia wengine wa Sudan wamekwama nchini humo bila maji safi ya kunywa, umeme, chakula na hata matibabu huku wengine wakitenganishwa na familia zao kufuatia mzozo huo unaoendelea.

Wakaazi wa Sudan watumai makubaliano ya sasa yataheshimiwa

Sudan EU richtet humanitäre Luftbrücke in den Sudan ein
Baadhi ya Wakimbizi wa Sudan, wakijisajili katika shirika la kimataifa la uhamiaji IOM wakitaka kuingia EthiopiaPicha: Amanuel Sileshi/AFP

Katika eneo jirani la mji Mkuu wa Khartopum, Hussein Mohammed mkaazi wa huko anasema anatumai hatimae milio ya risasi itaacha kusikika. Raia mwengine Sawsan Mohammed alisema kwamba iwapo makubaliano hayo yataheshimiwa yatampa nafasi ya kuwaona wazazi wake walioko Omdurman ikiwa ni upande wa pili wa Mto Nile.

Burhan amfuta kazi Dagalo kama Naibu wa Baraza Tawala Sudan

Wiki iliyopita picha za setilaiti zilionyesha moshi mkubwa uliokuwa ukifuka katika soko moja la Omdurman, huku watu wakikimbia katika barabara za mji huo wakitafuta mahala salama pa kutorokea. Afisa Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada ya kiutu Martin Griffiths ametaka pande hizo mbili zinazozozana kuheshimu kanuni za makubaliano yaliyofikiwa ili kutoa nafasi ya misaada inayohitajika kwa haraka kuwafikia walengwa.

Papa Francis ahimiza amani Sudan

Tarehe 15 Aprili, vita vilizuka nchini Sudan kati ya pande mbili hasimu za kijeshi, ile iliyotiifu kwa Kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Abdel-Fattah Burhan, na wengine walio watiifu kwa kiongozi wa kikosi chenye nguvu cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo. Vita vyao vya kugombania uongozi vimeziweka nchi jirani katika hali ya wasiwasi.

Huku hayo yakiarifiwa kiongozi wa zamani wa waasi Malik Agar, aliyechukua nafasi ya Dagalo kama Naibu wa Baraza la Uongozi nchini Sudan, alisema siku ya Jumamosi kwamba anajitahidi kusitisha mapigano. Agar amesema uthabiti wa Sudan unaweza kupatikana tu na wataalamu pamoja na jeshi lililoungana.

Chanzo: Reuters/ap