Makubaliano ya kusitisha vita yaleta matumaini mapya Sudan
21 Mei 2023Makubaliano ya kuweka chini silaha yamesainiwa na jeshi rasmi pamoja na kikosi cha dharura cha RSF baada ya mazungumzo yaliyofanyika kwenye mji wa Jedah nchini Saudi Arabia chini ya usimamizi wa kimataifa. Taarifa iliyotolewa Jumamosi jioni imesema kwamba makubaliano hayo, yanakusudia kuwapa watu wa Sudan nafasi ya kupata misaada ya kiutu. Licha ya makubaliano hayo, wakaazi wa mji mkuu Khartoum wameendelea kushuhudia mashambulizi ya hapa na pale leo Jumapili.
Matangazo ya kusitisha vita tangu mzozo ulipoanza Aprili 15 nchini Sudan, yameshindwa kusimamisha vita lakini makubaliano ya mjini Jeddah yanatoa matumaini mapya kwakuwa hii ni mara ya kwanza kwa pande hasimu kutia sahihi baada ya mazungumzo.
Wachambuzi wanasema bado haijawa wazi ikiwa Mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan au kamanda wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, watafanikiwa kweli kusitisha mapigano. Hakuna aliyehudhuria mazungumzo ya Jeddah kati yao.
Soma zaidi:Mashambulizi makali ya angani yatikisa Khartoum tena
Mzozo wa Sudan tayari umeshasababisha zaidi ya watu milioni 1.1kuyakimbia makazi yao kuelekea maeneo mengine ndani na nje ya Sudan hali inayochochea mgogoro wa kiutu kikanda.
Huduma za jamii zaendelea kuzorota
Wakaazi waliosalia Sudan wanapambana kuishi huku wakikabiliwa na uporaji, hali mbaya ya huduma za afya, usambazaji mdogo wa chakula mafuta, umeme na maji.
Wapatanishi kwenye mazungumzo ya Jeddah wanasema mazungumzo zaidi yatahitajika ili kuyaondoa majeshi katika maeneo ya mijini katika juhudi za kurejesha amani ya kudumu kwa kuwahusisha raia.
Jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Sudan Yassir al-Atta aliiambia televisheni ya taifa ya Sudan kuwa jeshi rasmi limekuwa likijaribu kuwaondoa wapiganaji wa kikosi cha RSF kwenye maeneo ya makaazi ya watu, shule na hospitali.
Mamilioni ya raia wamekwama wakati jeshi likifanya mashambulizi ya anga na mabomu likilenga vikosi vya RSF vilivyojiambatanisha kwenye makazi ya watu tangu mwanzo wa mapigano