1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu ya nchi duniani hazina mifumo ya tahadhari ya majanga

13 Oktoba 2022

Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari kuwa nusu ya nchi zote ulimwenguni bado hazina mifumo ya kisasa inayohitajika ya kutoa tahadhari dhidi ya majanga kuepusha vifo na maafa mengine.

https://p.dw.com/p/4I7Zk
Venezuela I Flut in Las Tejerias
Picha: Matias Delacroix/AP/picture alliance

Kulingana na ripoti hiyo, nchi ambazo mifumo yao ya tahadhari ni dhaifu, hukumbwa na maafa makubwa mara nane zaidi ikilinganishwa na nchi zilizo na mifumo bora ya tahadhari.

Tahadhari za mapema kuhusu mafuriko, ukame, mawimbi ya joto, vimbunga au majanga mengine huruhusu nchi kuweka mipango na mikakati muhimu inayohitajika kupunguza madhara mabaya.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema majanga kutokana na hali mbaya ya hewa yataendelea kutokea. Lakini hayapaswi kusababisha maafa mabaya.

Karibu nusu ya Ulaya katika hatari ya kukabiliwa na ukame

Kwa hivyo nchi zinapaswa kujihami na mifumo ya kutahadharisha kuhusu majanga mbalimbali. Cha kusikitisha ni kwamba ni nusu tu ya mataifa yote ya ulimwengu yaliyo na mifumo hiyo kwa sasa. Ripoti hiyo ya uchunguzi imeeleza.

Kanda ya Kenya, Somalia na Ethiopia hukumbwa na ukame ambao mara nyingi husababisha maafa ikiwemo vifo vya watu na mifugo.
Kanda ya Kenya, Somalia na Ethiopia hukumbwa na ukame ambao mara nyingi husababisha maafa ikiwemo vifo vya watu na mifugo.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kanda maskini huathiriwa zaidi

Kanda maskini ndizo aghalabu huwa katika hatari kubwa ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na majanga mengine asilia. Nchi katika kanda hizo hazina mifumo hiyo ya tahadhari.

Ripoti: Shirika la Oxfam lasema njaa inayochochewa na hali mbaya ya hewa yaongezeka zaidi ya maradufu katika nchi zilizoathirika.

Mami Mizutori ambaye ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia upunguzaji wa majanga ametoa wito kwa nchi kuwa na mifumo hiyo kwa dharura ili kunusuru uhai wa watu, wa viumbe vingine na mali.

Huku vitisho vikiongezeka, mifumo ya tahadhari imesaidia kwingineko kupunguza pakubwa vifo vinavyosababishwa na majanga.

Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya watu walioathiriwa na majanga iliongezeka karibu maradufu kutoka wastan wa 1,147 katika jumla ya 100,000 kila mwaka kati ya 2005 na 2014, hadi watu 2,066 kuanzia 2012 hadi 2021.

Mwanamke alia huku akimtafuta jamaa yake aliyepotea baada ya mafuriko kukumba eneo la Las Tejerias nchini Venezuela Oktoba 9, 2022.
Mwanamke alia huku akimtafuta jamaa yake aliyepotea baada ya mafuriko kukumba eneo la Las Tejerias nchini Venezuela Oktoba 9, 2022.Picha: Matias Delacroix/AP Photo/picture alliance

Aidha, idadi ya watu waliouawa au waliopotea baada ya majanga kila mwaka, ilipungua kutoka 1.77 kwa kila 100,000 hadi 0.84.

Mizutori alitoa mfano wa mafuriko ya Pakistan ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 1,700 na kuacha theluthi moja ya nchi hiyo ikiwa sasa imefunikwa na maji.

Soma: UN: Mamilioni ya watoto,wanawake wapo hatarini Pakistan

Amesema kuwa lau mifumo ya tahadhari isingetumika, basi idadi ya vifo Pakistan ingeongezeka Zaidi.

Watu 500 wauawa kufuatia mafuriko Nigeria

Takriban watu 500 wamekufa Nigeria na wengine milioni 1.4 wamelazimika kuyahama makwao kufuatia mafuriko mabaya kuwahi kuikumba nchi hiyo kwa miongo mingi.

Lakini wakati majanga yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabia nchi, yakizidi kuongezeka ulimwenguni, Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari kuwa nusu ya nchi ulimwenguni kote, bado hazina mifumo ya kisasa inayohitajika ya kutoa tahadhari na kuepusha maafa. 

Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 87, ni miongoni mwa wale wamelazimika kuyakimbia makaazi yao nchini Nigeria kufuatia mafuriko. Zaidi ya watu milioni 2.1 wanakadiriwa kupoteza makaazi yao Nigeria kwa sababu ya mafuriko mabaya kuwahi kuikumba nchi hiyo.
Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 87, ni miongoni mwa wale wamelazimika kuyakimbia makaazi yao nchini Nigeria kufuatia mafuriko. Zaidi ya watu milioni 2.1 wanakadiriwa kupoteza makaazi yao Nigeria kwa sababu ya mafuriko mabaya kuwahi kuikumba nchi hiyo.Picha: Getty Images/AFP/P. Utomi Ekpei

Kulingana na serikali ya Nigeria maafa hayo yametokea nchini humo tangu mwanzo wa msimu wa mvua mapema mwaka huu. Mafuriko kutokana na mvua nyingi na miundombinu duni vimeathiri maeneo mengi ya taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika na kuzusha wasiwasi wa kuwa itaathiri pia upatikanaji wa chakula na hata kusababisha mfumuko wa bei ya bidhaa.

Afrika Magharibi katika hatari mbaya ya ukosefu wa chakula

Kupitia taarifa, Rhoda Ishaku Iliya, naibu mkurugenzi wa mawasiliano katika wizara ya kiutu nchini Nigeria amesema nyumba 45,249 zimeharibiwa na vilevile mashamba ya kilimo yenye ukubwa wa hekari 70,566 nayo yameharibiwa kabisa.

Wakulima wa mpunga wametahadharisha kwamba mafuriko hayo huenda yataathiri bei ya nafaka hiyo.

Mwezi uliopita shirika la Mpango wa Chakula Ulimwenguni WFP Pamoja na shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, yalisema Nigeria ni kati ya nchi sita zinazokabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa kali.

(AFPE, )