1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Niger yawatimua mabalozi wa nchi 4 ikiwemo Ujerumani

Sylvia Mwehozi
26 Agosti 2023

Viongozi wa kijeshi wa Niger wametoa masaa 48 kwa mabalozi wa Ufaransa, Ujerumani, Nigeria na Marekani kuondoka nchini humo, wakati mvutano ukizidi kuongezeka kuhusu tishio la hatua za kijeshi kutoka ECOWAS.

https://p.dw.com/p/4VbHz
Niger | Maandamano
Wafuasi wa mapinduzi wakiwa wamekusanyika kwa maandamano mbele ya kambi ya Ufaransa huko NiameyPicha: Balima Boureima/picture alliance/AA

Viongozi wa kijeshi wa Niger wametoa masaa 48 kwa mabalozi wa Ufaransa, Ujerumani, Nigeria na Marekani kuondoka nchini humo. Hatua hiyo inakuja wakati mvutano ukizidi kuongezeka kuhusu tishio la hatua za kijeshi kutoka kwa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS.

Katika barua tofauti kwa serikali za nchi hizo, wizara ya mambo ya nje ya Niger imesema uamuzi huo umetokana na hatua ya mabalozi wa nchi hizo kukataa mwaliko wa serikali kwa ajili ya mkutano wa Ijumaa na hatua nyingine za serikali zao kinyume na maslahi ya Niger.

Soma : ECOWAS yakubaliana mpango wa uwezekano wa kuingilia kati Niger

Hata hivyo Ubalozi wa Ufaransa nchini Niger umelikataa tangazo hilo ukisema kuwa Paris, hautambui mamlaka ya watawala wa kijeshi. Hatua ya maafisa hao ni ya hivi karibuni zaidi katika uhusiano unaozidi kuzorota kati ya utawala mpya wa Niger na madola kadhaa ya nchi za Magharibi, pamoja na jumuiya ya ECOWAS.

Ufaransa imeunga mkono mara kwa mara wito wa ECOWAS wa kutaka kurejeshwa madarakani kwa rais Mohamed Bazoum, ambaye alipinduliwa Julai 26.

Siku ya Ijumaa jioni, wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa ilisema, "wapinzani hawana mamlaka ya kufanya ombi hili, kibali cha balozi kinakuja tu kutoka kwa mamlaka halali zilizochaguliwa za Niger."

Niger Niamey | Abdourahamane Tiani
Mtawala mpya wa kijeshi wa Niger Jenerali Abdourahamane Tiani,Picha: ORTN/Télé Sahel/AFP

Niger yaziidhinisha Mali, Burkina Faso kuisaidia kijeshi ikivamiwa

Ufaransa inao wanajeshi 1,500 walioko Niger ambao walikuwa wakimsaidia Bazoum katika vita dhidi ya wanamgambo ambao wanaendesha uasi wao nchini humo kwa miaka mingi, huku Marekani ikiwa na takriban wanajeshi elfu moja nchini humo.

Mapema Ijumaa, ECOWAS iliwataka viongozi wa mapinduzi wa Niger kufikiria upya msimamo wao na kushinikiza kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, huku tishio la nguvu likiwa bado "juu ya meza".

Viongozi wa kijeshi wa Niger pia wameonya dhidi ya uingiliaji kati wowote, wakishutumu ECOWAS kushirikiana na nchi ya kigeni ambayo haikutajwa jina.

Siku ya Alhamis nchi hiyo ilikubaliana na serikali za nchi jirani za Mali na Burkina Faso kuruhusu wanajeshi wake kuingia katika ardhi ya Niger endapo kutakuwa na jaribio lolote la kichokozi.