Niger yakumbwa na kitisho cha "mapinduzi ya kijeshi"
26 Julai 2023Wanajeshi hao wa kikosi cha ulinzi wa rais walimzuia kiongozi huyo ndani ya makazi ya rais na baada ya mazungumzo ambayo hata hivyo haikuwa wazi yalihusu nini kuvunjika "walikataa kumwachilia rais, hii ikiwa ni kulingana na chanzo kilichoongeza kuwa wanajeshi hao walipewa muda na jeshi wa kuachana na jaribio hilo.
Ujumbe uliochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter wa ofisi ya rais ulisema walinzi hao walionekana kuwa na hasira, ambapo pamoja na jaribio hilo wajaribu bila ya mafanikio kutaka kuungwa mkono na jeshi la kitaifa na walinzi wa kitaifa.
Soma Zaidi:Tawala za kijeshi Afrika magharibi, zataka zirudishwe ECOWAS
Duru zimesema rais yuko salama na kuongeza kuwa yeye na familia yake wako salama kwenye makazi yake. Chanzo hicho kimesema bado haijulikani sababu za walinzi hao kuchukua hatua kama hiyo na kile kilichojadiliwa kwenye mazungumzo hakijajulikana.
Mbunge wa chama cha Bazoum cha PNDP amesema amezungumza na rais na marafiki zake mchana wa leo na kusema wako salama. Bazoum aliyechaguliwa kidemokrasia mwaka 2021 ni mshirika wa karibu wa Ufaransa.
Jamii za kimataifa zalaani tukio hilo.
Jumuiya ya Maendelea kwa mataifa ya Magharbi, ECOWAS imelaani kile ilichoita jaribio la mapinduzi. Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo amesema wanafuatilia kwa karibu na watafanya kila lililo ndani ya uwezo wa mamlaka zao kuilinda demokrasia na kuongeza kuwa hawakubaliani na hatua yoyote itakayozuia utendaji mzuri wa mamlaka halali nchini Niger ama sehemu yoyote ya Afrika Magharibi.
Umoja wa Afrika nao umelaani jaribio hilo na mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Umoja huo Moussa Fakhi Mahamat amesema kupitia mtandao rasmi wa kijamii kwamba amefahamishwa kuhusu jaribio la baadhi ya wanajeshi walitaka kudhoofisha uthabiti wa taasisi za kidemokrasia na za kijamhuri nchini Niger akilifananisha na jaribio la mapinduzi ya kijeshi.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell naye amesema umoja huo una wasiwasi mkubwa juu ya matukio ya huko nchini Niger. Kwenye taarifa yake amesema Umoja wa Ulaya ulaani jaribio lolote linalolenga kuvuruga demokrasia na kutishia utulivu wa Niger.
Taifa hilo la Afrika Magharibi ni moja kati ya mataifa ulimwenguni yasiyo na utulivu, na hasa baada ya kushuhudia mapinduzi ya mara nne tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mnamo mwaka 1960, pamoja na majaribio kadhaa ya kupindua mamlaka.
Mapinduzi ya mwisho kufanyika nchini humo ni ya mwaka 2010, yaliyomuondoa mamlakani aliyekuwa rais Mamadou Tandja. Hata hivyo, kulikuwa na jaribio la mapinduzi siku kadhaa kabla ya shughuli za uapisho wa Bazoum Aprili 2021, hii ikiwa ni kulingana na vyanzo vya kiusalama vya wakati huo.
Baadhi ya watu walikamatwa ikiwa ni pamoja na aliyehisiwa kuwa kiongozi wa jaribio hilo, Sani Gourouza aliyekuwa kapteni wa kikosi cha anga cha nchini humo. Alikamatwa akiwa nchi jirani ya Benin na kukabidhiwa kwa mamlaka ya Niger. Waziri wa zamani wa mambo ya ndani Ousmane Cisse, aliyehudumu katika serikali ya mpito kati ya mwaka 2010-2011, alizuiliwa kizuizini mwaka 2022 kutokana na jukumu lake kwenye jaribio hilo.
Aliachiliwa huru Februari mwaka huu, lakini wenzake watano ikiwa ni pamoja na Gourouza walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
Jaribio la pili la kumuondoa Bazoum lilifanyika mwezi Machi mwaka huu, wakati rais alipokuwa Uturuki, amesema afisa mmoja wa Niger. Lakini mamlaka hazikutangaza hadharani tukio hili.
Januari 2018, mahakama ya kijeshi iliwahukumu wanajeshi 9 pamoja na raia kifungo cha kati ya miaka mitano hadi 15 jela kwa jaribio la kumpindua mtangulizi wa Bazoum, Mahamadou Issoufou mwaka 2015. Waliohukumiwa ni pamoja na Jenerali Souleymane Salou, aliyewahi kuwa mkuu wa utumishi na mmoja ya afisa wa utawala wa kijeshi uliompindua Tandja, mwaka 2010.
Soma Zaidi:Umoja wa Mataifa: Hali ya usalama Afrika Magharibi na Sahel inazidi kuzorota