1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya na ukaguzi wa muda wa mipakani kukabili wahamiaji

11 Septemba 2024

Umoja wa Ulaya unakabiliwa na ongezeko la wahamiaji halali na wengine haramu, na hivyo kupelekea baadhi ya nchi wanachama kuanzisha upya ukaguzi wa mipakani ndani ya eneo la Schengen.

https://p.dw.com/p/4kUo8
Polisi wa Ufaransa wakifanya ukaguzi
Polisi wa Ufaransa wakifanya ukaguziPicha: Pascal Rossignol/REUTERS

Sheria za makubaliano ya Schengen zinaruhusu nchi wanachama kuanzisha ukaguzi wa mipakani "kama suluhu la mwisho" ili kuepusha tishio kubwa kwa usalama wa ndani au sera ya umma kwa taifa husika. Austria imerejesha ukaguzi wa mpakani na majirani zake Slovakia na Jamhuri ya  Czech hadi Oktoba 15 mwaka huu huku Slovenia ikichukua hatua hiyo dhidi ya Hungary hadi Novemba 11.

Soma: Ujerumani yaijaribu EU kwa kuongeza udhibiti mipakani

Denmark nayo imeanzisha ukaguzi wasafiri wa nchi kavu na baharini kutoka Ujerumani hadi Novemba 11, na kutetea uamuzi wake kutokana na shinikizo kwenye mfumo wa kupokea waomba hifadhi, wasiwasi wa kiusalama unaochochewa na makundi ya kigaidi hasa kutokana na vita vya Gaza pamoja na vitendo vya kukidhalilisha kitabu kitakatifu kwa waislamu cha Quran mnamo mwaka 2023. Serikali mjini Copenhagen imeelezea pia kitisho cha mitandao ya wahalifu wanaohusishwa na vita nchini Ukraine ikiwa ni pamoja na hatari za vitendo vya ujasusi kutoka Urusi.

Polisi wa Ujerumani na ukaguzi wa mipaka
Polisi wa Ujerumani na ukaguzi wa mipakaPicha: Christoph Hardt/Panama Pictures/IMAGO

Kwa upande mwingine, Ufaransa ilitaja pia shinikizo kwenye mfumo wa mapokezi na vitisho vya ugaidi ili kurejesha ukaguzi kwenye mipaka yake na nchi za Schengen, ambao utadumu hadi Oktoba 31 mwaka huu.

Ujerumani nayo inapanga kuanzisha mnamo Septemba 16 na kwa muda wa miezi sita, udhibiti mkali zaidi wa mipaka yake ya ardhini hasa na mataifa ya Poland, Jamhuri ya Czech na Uswisi. Serikali mjini Berlin imesema udhibiti kwenye mpaka wake na Austria uliwezesha kuwarejesha wahamiaji wapatao 30,000 tangu Oktoba mwaka 2023.

Ukaguzi wa mpakaniulioanzishwa na Italia dhidi ya Slovenia unatarajiwa kudumu hadi Desemba 18, baada ya serikali mjini Rome kuashiria hatari ya magaidi kujificha miongoni mwa wahamiaji wanaotumia njia ya Balkan, pamoja na wasiwasi juu ya vita vya Ukraine na uwezekano wa kutokea vurugu zinazohusishwa na Italia kushikilia urais wa kupokezana wa kundi la mataifa saba yaliyoinukia kiuchumi duniani G7.

Ujerumani: Rasimu ya kuwarudisha watu katika mataifa yao

Norway, ambayo si mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) lakini iliafiki makubaliano ya Schengen, imerejesha udhibiti wa mpakani hadi Novemba 11 katika bandari na kivuko kinachoonganisha nchi hiyo na mataifa ya Schengen kutokana na kile ilichosema kuwa ni kitisho cha operesheni za kijasusi za Urusi zinazotishia usafirishaji wa Norway kwa msaada wa gesi au kijeshi kwa Ukraine.

Soma: UN yaonya kuhusu sera ya uhamiaji ya nchi za Ulaya

Slovenia imechukua hatua kama hiyo dhidi ya majirani zake Croatia na Hungary hadi Desemba 21, ikitaja kuzorota kwa hali ya usalama nchini Ukraine na Mashariki ya Kati, tishio kubwa la ugaidi, na uhalifu uliopangwa katika eneo la Balkan Magharibi.

Sweden imeimarisha ukaguzi wake wa mpakani hadi Novemba 11, ikitaja ongezeko la hatari ya kutokea vurugu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi yanayo fungamanishwa na chuki dhidi ya wayahudi kutokana na mzozo wa Gaza.

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

Soma: Watu 830,000 wakaguliwa mipakani Ujerumani kwa siku 21

Finland nayo ilifunga mpaka wake wa ardhini na Urusi kwa muda usiojulikana huku bandari kadhaa zikiwekwa pia kwenye orodha hiyo ili kukabiliana na ongezeko la wanaotafuta hifadhi. Serikali mjini Helsinki iliishutumu Moscow kwa kuchochea ongezeko hilo, taarifa iliyokanushwa na Ikulu ya Kremlin.

Makubaliano ya Schengen yalisainiwa mwaka 1985 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1990 na yanayajumuisha mataifa 29 ili kuunda eneo moja linaloruhusu usafiri wa watu na bidhaa bila ya uwepo ukaguzi wowote mipakani.